Maafisa wa Kukabili Ugaidi, waruhusiwa kumzuilia kwa siku 15 dereva wa gari lililokuwa limewabeba madaktari wawili wa Cuba

Maafisa wa Kukabili Ugaidi, ATPU wameruhusiwa kumzuilia kwa siku 15 dereva wa gari lililokuwa limewabeba madaktari wawili wa Cuba waliotekwa nyara Ijumaa wiki iliyopita na watu wanaoshukiwa kuwa wa kundi gaidi la Alshabab.
 
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Milimani, Muthoni Nzibe,  ametoa agizo hilo baada ya upande wa mashtaka kuomba kwamba mshukiwa Isaack Ibrein Robow anapaswa kuzuiliwa zaidi kuruhusu uchunguzi.
 
Mshukiwa alikamatwa tarehe 12 mwezi huu Mjini Mandera kisha kusafirishwa hadi jijini Nairobi Jumapili wiki hii ili kufikishwa mahakamani.
 
Idara ya uchunguzi inalenga kujua iwapo mshukiwa alishirikiana na magaidi kufanikisha utekaji nyara wa madaktari hao. Iwapo atapatikana na hatia, atahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.
 
Haya yanajiri huku madaktari wanne wa Cuba waliokuwa wakihudumu katika Kaunti za Lamu na Tana River  wakiondoka eneo hilo kwa kuhofia usalama wao. 

Wikendi, madaktari wawili wanne waliokuwa wakihudumu katika Kaunti  za Garrisa na Wajir walisafirishwa hadi hapa Nairobi baada ya wenzao wawili waliokuwa wakihudumu katika Kaunti ya Manderea kutekwa nyara.

Maafisa wa usalama  kwa sasa wanaendelea juhudi za kuwakomboa wawili hao Landy Rodriguez na Assel Herera Correa ambao walivushwa nchini Somalia baada ya kutekwa nyara Ijumaa wiki iliyopita.

Kundi la wazee ni miongoni mwa wanaohusika katika juhudi hizo ambazo vilevile zinawashirikisha maafisa wa jeshi la Kenya KDF, na polisi kutoka vitengo mbalimbali vya kukabili uhalifu.

Related Topics