Sajenti Mstaafu Aron Ojode anajulikana kwa majina ya utani kama Jabunde (mtu wa Bunduki) ama Jalweny (Mwanajeshi) na wakazi wa Kijiji cha Majiwa eneo la Kochia kwenye Kaunti ya Homabay. Mzee Ojode, mwenye Umri wa miaka 78, alihudumia taifa kama mwanajeshi kwa miaka 22 huku kilele cha huduma yake ni kwamba alichaguliwa kati ya maafisa 28 waliohojiwa kusimamia ulinzi wa kaburi la Rais wa Kwanza wa Jamuhuri Mzee Jomo Kenyatta mnamo mwaka wa 1978.
Mwanajeshi huyo mstaafu anakumbuka jinsi Mkuu wa Majeshi wakati huo marehemu Jenerali Jackson Mulinge alivyomkabidhi wajibu huo kama afisa wa kwanza kusimamia alipolazwa Mzee Kenyatta na akapewa idhini na bunge kutekeleza wajibu huo kwa muda wa miaka minne.