Matiang'i, awataka Wakenya kuzitumia bidhaa zinazotengenezwa humu nchini

Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi, Fred Matiang'i,amesema Kenya imeweza kuhifadhi shilingi milioni 700 kufuatia ushonaji wa sare mpya za maafisa wa polisi humu nchini.

Akizungumza jijini Nairobi alipokagua sare hizo, Matiang'i amesema kuwa sare 1000 hutengenezwa kila siku na Shirika la Huduma kwa Vijana NYS.

Vilevile Matiang'i  amewataka Wakenya kuzitumia bidhaa zinazotengenezwa humu nchini ili kuboresha uchumi wa taifa, na ni sharti hulka ya kuagiza bidhaa kutoka mataifa ya nje ikomeshwe.

Mwaka jana Matiang'i alitangaza kuwa sare hizo mpya za maafisa wa polisi zitatengenezwa humu nchini baada ya kuzinduliwa rasmi na Rais Kenyatta.

Amesema serikali itashirikiana na sekta ya binafsi, ili kuhakikisha bidhaa zinazotumika zinatengezwa nchini.

Wakati uo huo, amesema serikali itaanzisha msako dhidi ya wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa lengo la kupiga jeki sekta ya viwanda.

Kauli hiyo imetiliwa mkazo na Waziri wa Vijana na Jinsia Margaret Kobia aliyeanadamana naye.

Related Topics