Alilipwa kumchapa Raila, Mvurya kwa fimbo lililogangwa

Mzee Lengo (katikati) baada kuwachapa kiongozi wa ODM Raila Odinga (kushoto) na Gavana Salim Mvurya (kulia). [Picha: Hisani]

Jina la Mzee Karisa Lengo Mdzomba lilichipuka mnamo mwezi Septemba mwaka 2014 baada ya kustahimili uoga na mzizimo wa hofu kupasua umati wa watu katika hafla ya hadhara na kuwatwanga bakora za mpwito kinara wa ODM Raila Amolo Odinga na gavana wa Kwale, Salim Mvurya.

Hadi leo, siyo kinara wa upinzani Raila Odinga wala gavana wa Kwale Salim Mvurya anayeweza kutueleza walipata viboko vingapi vya Lengo Mdzomba kutokana na upesi wa wepesi wake katika ujuzi wa kutumia fimbo hiyo iliyozua majadiliano ya faragha kote nchini wakati huo.

Viongozi wa mashinani wa chama cha ODM, James Dena (akiwa mwenyekiti wa tawi la Kinango na mwenzake Hassan Chitembe wa Matuga) ambao ndio waliokuwa miongoni mwa waandalizi wa ziara ya Raila Odinga mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa 2013, wanasimulia kisa hicho kama cha kujuvya mjuvyo wa maswali ya usalama wa viongozi wakuu.

Ijapo waliocharazwa bakora hizo hawakumbuki ni fimbo ngapi ziliwaangukia, Dena na Chitembe ambao ndio watu wa kwanza kumshika na kumzuia Karisa Lengo Mdzomba asiendelee kuwaadhibu viongozi, wanakumbuka kwamba walimsikia mwenyewe akitoboa kuwa aliwachapa bakora sita kwa mpigo (kila mmoja akikula tatu za haraka-haraka).

Hatimaye alikamatwa na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 5000 na hakimu mkazi wa Kwale wakati huo, Christine Njagi kwa kosa la kuhatarisha amani baada ya kinara wa ODM Raila Odinga  na gavana wa Kwale kumsamehe kwa tendo lake potofu.

Hii ni baada ya washauri wa Raila wakiwemo Wazee wa jamii ya Waluo kumshauri kwamba dawa ya moto ni moto kwa kuwa tukio lolote lile la aina hiyo huwa silo la kawaida ile kutatuliwa na Wazee njenje. Wazee njenje kwa lugha ya kitamaduni za jamii waamini wa ndumba, ni mtafakari wa asilia za ramli ili kujua kinaga ubaga wa chanzo cha jambo fulani kutoka kwa wataalamu wa kiasili kwenye jamii.

Bakora ya ajabu

Habari ambazo zimejitokeza sasa ni kuwa bakora ya Mzee Karisa Lengo Mdzoma kamwe haikuwa ya kawaida kwani licha ya kutumiwa na Lengo, ilikuwa imepitia mikono kadha wa kadha ikiwemo ya wanasiasa washirikina ambao waliidhinisha kichapo cha kinara wa ODM na gavana wa Kwale kwa lengo la kuamini kwamba urogi walioufanyia fimbo ama bakora hiyo, utamlemaza umaarufu wa kisiasa wa Raila.

Walivyodanyanywa na waganga wao ama wachawi kama wanavyoamini hao wenyewe ni kuwa wakati uchungu wa bakora ile ukimwingia kinara Raila Odinga mwilini, ungemdhuru kwa kujiwa na mikosi na visanga na hata kuamua kuachana na siasa ya kitaifa, wanasiasa hao wakiogopa kwamba angekuwa tisho kubwa la serikali ya UHURUTO katika uchaguzi wa 2017.

Hii ni baada ya shinikizo la OKOA KENYA kuanza chini ya mrengo wa CORD kwamba marekebisho ya katiba lazima yapendekezwe kukabili hali ilivyo ya kisasa baada ya Raila na Kalonzo kushindwa katika uchaguzi mkuu wa 2013.

Seneta mmoja wakati huo ambaye kwa sasa amefanikiwa kuchaguliwa gavana katika uchaguzi mkuu wa 2017 na mwenye ufahamu mkubwa wa ngonjera za uchawi katika mwambao wa pwani ya Kenya, alishawishi miongoni mwa wanasiasa wengine wanaoamini uchawi kuwa upo kuzua wazo la jinsi wangeweza kumwadhibu kinara wa ODM ili kasi yake ya siasa ipungue.

Ni dhahiri wazi kuwa hatua ya kichapo hiki ilipangwa kisiasa kama Mzee Lengo mwenyewe anavyothibitisha wakati akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa amezuiliwa akiwa Kwale;

“Nilisukumwa kutenda hivyo na shinikizo la mrengo wa CORD chini ya mpango wake wa Okoa Kenya. Wamekuwa wakiitisha mikutano mingi wakisema wataiokoa Kenya, kwani nchi hii imeokolewa mara ngapi? Anukuliwa akijitetea wakati huo ili kuficha lengo la wanasiasa kutumika licha ya kuwa jibu lake tosha kuona uhusiano wa kisiasa hapo.

Kudhihirisha ukweli wa kuhusika kutumiwa na mrengo wa Uhuruto, Lengo Mdzomba alisahau akatoboa hivi; “Jomo Kenyatta aliongoza taifa kujikomboa kutoka kwa wakoloni kama mkombozi wa kwanza sasa itakuwaje mambo ya Okoa Kenya ilhali hata serikali ya Uhuruto haijamaliza hata miaka mitatu (2014). Rais Uhuru Kenyatta hana hata muda wa kupanga mikakati ya maendeleo ya nchi kwa sababu ya mikutano hii yao,” azidi kunukuliwa mcharaza kiboko.

“Sikujua vile nilivyopandwa na mori hadi kuwachapa, mimi nilijiona tu watu wamenizuia na bakora yangu kunyakuliwa,” asimulia Lengo.

Malipo ya milioni 2

Kulingana na mshirika wa ndani katika mpango huo ambaye jina lake tumelibana, watu fulani walichaguliwa kumtafuta mtu atakaye kabidhiwa fimbo itakayogangwa ya kumcharaza Raila na wale wanasiasa wanaoishi kwa nguvu za uchawi kutafuta huduma za watakaosaidia kuroga fimbo itakayotumika.

Wanasiasa walipofanikiwa kushauriana na waganga wao, hatujui ni utapeli ama ni tamaa tu ya hela za bwerere, na kumpata mshenga (mtumwa) wa kutumia fimbo ama bakora ile, walikusanyika kwenye hoteli moja ya kifahari wiki moja kabla ya ziara ya kiongozi wa upinzani ya pwani mwishoni mwa mwezi Septemba 2014.

“Sisi tulikuwa na jukumu la kumtafuta mtu shujaa ambaye anaweza kujitoa mhanga kutumia bakora ile na ijapo shabaha yetu alikuwa ni Raila Odinga, tulionelea Lengo Mdzomba pia amcharaze viboko gavana Salim Mvurya sawia na Raila ndio isionekane kwa haraka kwamba imepangwa kisiasa,” asimulia mmoja wa wale waliomtafutia kazi Mzee Lengo.

Kulingana na msemaji huyu, wanasiasa waliomzingira Seneta mdhamini wa fimbo hiyo, hawakuwa wa mrengo wa serikali ya Uhuruto tu bali hata vibaraka wa CORD ambao walikuwa wamewekelea maguu yao mawili, moja kwa CORD na lingine serikalini. Miongoni mwa listi ya wanasiasa hawa ni pamoja na wabunge, wawakilishi wa kina mama waliochaguliwa wabunge sasa na wengine kuanguka katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Mzee Lengo Mdzomba hakualikwa kwenye kikao cha wanasiasa na seneta (sasa gavana wa kaunti moja nchini) ila wale waliotumwa kwa waganga na kwa mtumiaji wa fimbo (Lengo) ndio walioshuhudia mpango na malipo ya kazi nzima hiyo.

“Nilitambulishwa kama mtu niliyempata Lengo na mwenye kumpelekea bakora ile lakini hata mimi sijui kama ilikuwa imepitia kwa mganga ama vipi, mimi ilikuwa ni kumpelekea bakora na malipo yake na kumuongoza jinsi ya kutekeleza kazi yake,” atugusia mmoja wa wahusika wa karibu kwenye mpango huo.

Matapeli wa 1.8 milioni

Ukweli wa mambo ni kwamba kazi yote hii ilimgharimu seneta jumla ya shilingi milioni 2 lakini hata yeye mwenyewe hakujua kuwa Mzee Lengo ambaye alikuwa shujaa wao baada ya kuona vyombo vya habari jioni hiyo kuwa kazi imefanywa, atatapeliwa na wanasiasa alipwe tu shilingi elfu 20 huku wakimeza zote shilingi milioni moja na laki nane (1.8 milioni).

“Nilishuhudia milioni mbili tukiwekewa mezani na seneta na ijapo mimi nilipata nilichostahili kulipwa kwa kumtafuta mcharazaji wa viboko, sikufurahia malipo aliyolipwa Mzee Lengo kwani kitita chote kilitapeliwa na wanasiasa tuliokuwa nao kwenye mipango hii,” atoboa jamaa huyu tuliyebana jina lake.

Mzee Lengo Karisa anahojiwa na walinzi wa Raila Odinga. [Picha: Hisani]

Madhara ya bakora ya Lengo Mdzomba

Wiki moja baada ya Raila Odinga kucharazwa bakora na Lengo, mwenyekiti wa Wazee wa jamii ya Waluo wakati huo aliitisha kikao cha dharura kuthakimini chanzo cha mtu wa akili timamu kama Lengo Mdzomba kuamua kumchapa bakora mtoto wao. Walihisi kwamba bila shaka kunao uwezekano wa kisiasa ya mazingaombwe.

Yaaminika wazee hao nao kulingana na itikadi za kijamii waliitisha kikao cha dharura na kuandaa tambiko za kupambana ama kukinga maovu yoyote yale ambaye yangemuandama kinara wa ODM.

Pigo la Raila

Miezi minne baada ya kisa hiki, maadui wke waliomtakia mabaya walionekana wakifurahia bafuni (kimoyomoyo) kufuatia pigo la kufariki ghafula kwa kipenzi chake na familia nzima, kijana Fidel Odinga mnamo Januari 4 mwaka 2015.

Wadadisi wengi walizungumzia sana kuhusu matukio haya mawili lakini kwa kuwa Raila Odinga ni mpevu wa mambo mengi, aliwashinda nguvu wabaya wake muda wote huu ambapo amekuwa akitegwa akitegua.

Wakati akijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2017, halikadhalika, msichana wake ambaye wengi walimuona kama mrithi wa Fidel Odinga katika ndoto ya siasa ya eneo bunge la Kibra katika kaunti ya Nairobi naye aliugua kwa ghafula bila ya matarajio ya wengi. Rosemary aliugua maradhi ya kichwa na hivi tusemavyo ameathirika macho baada ya kutibiwa kwa uda mrefu katika hospitali moja ya Afrika Kusini.

Licha ya siasa safi na umaarufu mkubwa katika mrengo wa NASA, Raila alishindwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita lakini sasa ameanza kunawiri tena akijiguagua kwa 2022.

Laana kwa Lengo

Wale ambao wanamwamini sana kinara wa ODM, wanasema kwamba huyu amefikia kiwango cha kuheshimika kama baba wa taifa nay ale ambayo yanamwaandama sasa Mzee Lengo Mdzomba ni kana kwamba amelaaniwa na ‘Baba’.

Ushujaa wake wa 2014 baada ya kumchapa Raila bakora ulififia punde tu aliposamehewa. Kwanza wanasiasa waliomtumia walimrusha baki ya pesa ya shilingi elfu 30 ambayo alikuwa alipwe baada ya kazi.

Mara kwa mara, amekuwa akifadhiliwa na shirika la haki za kibinaadamu la Haki Afrika na ambalo hadi sasa bado linamnusuru. Lengo anasema kwa sasa hawezi kuzungumza wala kuchukua uamuzi wowote ule bila kushauriwa na shirika hili la Haki Afrika.

“Niliambiwa nisizungumze na vyombo vya habari ama mtu yeyote yule kuhusiana na suala hili la bakora. Ukitaka kuzungumza kuhusu suala hili, pitia kwa shirika la Haki Afrika”, huu ndio ujumbe wa hivi punde kutoka kwa Mzee Lengo Mdzomba ambaye anaishi maisha ya kivyake.