Kenyatta Caves: Makao ya mashujaa Jomo, Oginga na Pinto kabla ya uhuru

Mzee Jomo Kenyatta.

Upepo maridadi ukipiga katika kitongoji cha Mwanguwi kutoka msitu wa Mshomoto milima ya Sungululu kaunti ndogo ya Wundanyi.

Mguuni mwa milima hiyo utampata Mzee Charles Mlekenyi miaka 73 akisimama kwa korija lake la maua ya kupendeza ajabu katika shamba la ekari 9 aliloachiwa na mababu zake. Karibu na nyumba yake kuna kibao cha mbao kimesimama juu ya mlima kikiashiria ‘Jomo Kenyatta Caves’ ambacho huonekana vizuri hata kwa umbali.

Zamani yakijulikana kama mapango ya Kino, mapango hayo yalitumika kama maficho na rais wa kwanza wa jamuhuri ya Kenya Mzee Jomo Kenyatta kwa miaka akihepa kuwindwa na mabeberu wakati wa kupigania uhuru.

Makao ya mashujaa

“Mapango haya yaligeuka kuwa nyumbani kwa Mzee Kenyatta na yalikuwa salama kwake pamoja na wapiganaji uhuru wengine kutoka Kenya na Tanzania miaka ya 1950s,” alieleza Mlekenyi.

Licha ya miaka yake, Mzee Mlekenyi ana kumbukumbu zote za matukio hayo kutoka miaka ya 60s ambazo zingepelekea shamba lake kujulikana kimataifa kwa juhudi walizochangia wazazi wake kupigania uhuru.

Akielekea katika sehemu iliyotengwa na mwamba mkubwa, Mzee Mlekenyi anadumisha mazungumzo ya kusisimua kuhusu mashujaa walioishi kwenye mapango hayo. Anatambaa kuingia ndani ya pango kubwa lililo na mwanga hafifu. Ndani kuna upepo na baridi inayopiga kuogofya ikinuka vumbi na uzee. Mtu anaeza ogopa mizimu ya mashujaa waliokuja kita kambi yamekuja kama vivuli.

Mlekenyi anafichua kuwa pango hilo ni la kikomunisti ambamo mulilala mpiganaji uhuru wa Uganda Milton Obote na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutoka Tanganyika (Tananzia) ambao  walikuja mara kwa mara kushauriana na viongozi wa Kenya. Nyuma yake mna uwanja mkubwa na pango ambamo muliishi Mzee Kenyatta na wapiganaji uhuru wengine wa Kenya.

Milton Obote wa Uganda.

“Kenyatta aliishi kwenye pango la kibepari naye Obote na Nyerere kwenye pango la kikomunisti. Wakati wa migogoro hawangeishi pamoja kwani walitofautiana kwa falsafa za kiuchumi lakini wangekutana kushauriana juu ya uhuru wa nchi hizi tatu (Kenya, Tanzania na Uganda,” alieleza.

Mzee Julius Nyerere.

Mlekenyi alisema kufikia miaka ya 1950s, babake ambaye ni Mzee Zephania Nyambu Mwakio, mpiganaji uhuru kutoka Taita, aliwachukua wapiganaji uhuru kutoka sehemu za Kati ya Kenya, Kaskazini Mashariki, Bonde la Ufa, Magharibi, Mashariki na mikoa ya Pwani ambao walikuwa wakitafutwa na mabeberu. Wakiwemo, James Gichuru, Mbiu Koinange, Pio Gama Pinto, Paul Ngei, Fred Kubai, Mengo Woresha na Ronald Ngala. Wengineo ni Martin Shikuku, Masinde Muliro na Tom Mboya.

Jaramogi Oginga Odinga.

Mzee Mlekenyi ambaye alipewa jina la utani na watu mtaani kama kijana wa Kenyatta, alisema mamake, Sylvia Manga, alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Jomo Kenyatta kwani alikuwa mpishi wake kwa muda wote aliokuwa akiishi kwenye mapango. Mama Manga alizaliwa mwaka 1911 na akaaga dunia Januari mwaka 2015 akiwa na miaka 104.

Ndani ya chumba kilichotengwa kando ya nyumba, mali ya Jomo Kenyatta imehifadhiwa vizuri ikiwemo, kitanda cha ngozi ya mnyama, kigoda, kichana cha chuma na mashine ya kushona nguo yenye uzani wa kilo 40 ya kijerumani ambayo inasemekana alitumia kushona nguo zake akiwa Taita.

Sayansi ya kiafrika

Muda wa kuishi kwa mapango uliongezwa na mbuzi kuchinjwa mara kwa mara ili kutabiri siku zijazo. Hii ilikuwa kupitia kutafsiri utumbo ulivyojichora. Njia nyengine iliyoaminika sana ilikuwa kulisha mbuzi mti wa sumu kisha Kenyatta na wenzake wamzibe mdomo na pua kwa nguvu ili kumuua. Mbuzi ikifariki ingepigapiga chini kwa uchungu ikichora mchangani. Michoro hiyo pia ingetumika kama ile ya utumbo.

Mwakishaluwa Mwamburi, mwaguzi aliyejulikana vyema kwa kazi yake, angetafsiri ishara hizo kwenye utumbo na mchangani. Angetafsiri hatari zijazo na atoe ushauri nini cha kufanya. Mwakishaluwa pia alijulikana kwa uchunguzi wa mienendo ya wakoloni kutumia ujuzi wake. Ilikuwa moja ya uganga alipotabiri Kenyatta ndiye atakayekuwa Rais wa Kenya.

“Baada ya ufunuo huo, wengi walimwangalia mzee Mwakichaluwa kwa mamcho mabaya na kumchukulia tofauti sana,” alisema Mlekenyi.

Kibao kinacho waonyesha ishara wageni nje ya mapango ya Jomo Kenyatta mlimani Taita.

Mchango wa familia ya Nyambu

Mchango ambao familia ya Mzee Nyambu na mapango hayo ulitoa kupelekea uhuru wa Kenya umeleta mamia ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi kuzuru shamba wajionee mapango hayo. Makumbusho ya nchi yaliweka rasmi mapango hayo kama ukumbusho wa Kenya ukiwa na umuhimu kihistoria na hata kitamaduni una thamani kubwa.

Licha ya kuwa na jukumu zuri kwa kupigania uhuru wa Kenya, Mzee Mlekenyi alisema babake aliuliwa na mateso ya akili. Alisema wakati Mzee Jomo Kenyatta na wenzake kwa jina Kapenguria 6 wakiteseka jela, Mzee Zephania Nyambu alifungwa Shimo La Tewa miaka minane kwa kuwaficha wapiganaji uhuru wenzake.

Wakenya wengi leo hii hawajamtambua Zephania Nyambu kama shujaa licha ya kuwa pia aliona cha mtema kuni mfano wa wale mashujaa wenzake wa Kapenguria Six. Amini usiamini miaka hii minane ambayo Mzee Zephania Nyambu alikuwa Shimo la Tewa, ni marehemu Jaramogi Oginga Odinga ambaye alihakikisha familia hii imepata chakula.

Kulingana na Mlekenyi amabye yungali akikumbuka kimasomaso, Jaramogi aliwasaidia kwa kuwaletea chakula muda wote huo ambao baba yao alikuwa amefungwa Shimo la Tewa sawia na Jomo Kenyatta na wengine waliokuwa Kapenguria.

Mkutano na Kenyatta watibuka

Kenyatta alipokuwa rais wa Jamuhuri ya Kenya ujio wake wa Wundanyi ukaisha. Hata hivyo, mwaka 1978 Jomo Kenyatta aliteua kukutana na Mzee Nyambu lakini mkutano haukufanyika kwani Kenyatta alifariki kabla. Siku ambayo Nyambu alisafirishwa kukutana na rafiki yake wa dhati Jomo Kenyatta, ndiyo siku ambayo Jomo aliaga dunia huku akimsubiri hotelini mjini Mombasa.

Mzee Nyambu chini ya agizo la Jomo Kenyatta aliwasili mjini kumsubiria amalize ziara yake ya Msambweni, Kwale lakini kwa kuwa mpanga yote ni Mungu, mkutano wao ulitibuka kufuatia kifo cha ghafla cha kiongozi wa taifa huyo. Aliwajibika kurudi Taita shingo upande.

“Babangu hakuamini kifo cha Rais Kenyatta na akajua serikali haitamkumbuka kwa kazi yake aliyoifanya kusaidia kupata uhuru,” alisema. Babake Zephania Nyambu alikufa mwezi Agosti mwaka 1993.

Jitihada za Wazee wa Njavungo

Kama sehemu ya kuikumbuka familia ya Mzee Nyambu kwa nafasi iliyochukuwa katika kupigania uhuru, Njavungo, kikundi cha wazee wa Taita Taveta, kupitia mwenyekiti wao Ronald Mwasi alipanga kumkutanisha Sylvia Manga na Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2013. Mjane huyo aliomba gari la kumpeleka kanisani,, gari la waumini wa kanisa lake la Mama Silvia Church, kuku, ng’ombe na nyumba ya heshima (kisasa) yake ama familia ya kuishi.

“Rais aliguswa na hatma ya mama huyo (marehemu sasa) na akataka ajengewe nyumba yake,” alieleza Mzee Mwasi.

Baadaye, maafisa waandamizi wa serikali wakaandamana nyumbani kuangalia mahali pale palipostahili kujengwa nyumba. Migogoro ikazuka mahali pa kujenga nyumba Mlekenyi akisisitiza nyumba ijengwe nyumbani kwa kakake mdogo ambapo mama alikuwa akiishi mpaka kufa kwake. Katika tamaduni za Kitaita, kitinda mimba wa kiume ndiye hurithi boma kutoka kwa wazazi.

Miko ya jamii ya Wataita

Mlekenyi alisema ingekuwa kuvunja mwiko nyumba ya mama yake ijengwe kwa shamba lake ilhali mama aliishi na kitinda mimba wake umbali wa mita mia moja.

“Singeweza kukubali wajenge nyumba ya mama katika shamba langu ilhali mimi si kitinda mimba wala niliyekuwa nikiishi na mama. Nyumba ilistahili kujengwa mahali mama alipokuwa akiishi lakini hawakufanya hivyo,” alieleza.

Kaka yake mdogo, anayeitwa Mbiu Koinange jina la mmoja wa waliokuwa pamoja na Jomo Kenyatta mapangoni bado anaishi katika nyumba ya matope iliyozeeka pamoja na mke na watoto wake. Nyuma ya nyumba yake ni makaburi ya Zephania Nyambu, babake na Sylvia Manga, mamake.

Ni shambani pake ambako zawadi ya nyumba ya mama ingestahili kujengwa lakini ni miaka sasa na hawajaelewa hatima ya zawadi hiyo kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Hapa ndio nyumbani ambako sisi sote tumezaliwa na kulelewa, bado tunangoja kama zawadi hiyo kutoka kwa Rais itafika,” alisema.