Wauguzi wakiuka agizo la Rais Kenyatta la kusitisha mgomo

Wauguzi wanaogoma wamelikiuka wazi agizo la Rais Uhuru Kenyatta la kuwashurutisha warejee kazini. Hayo yanajiri huku Waziri wa Leba, Ukur Yatani na Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi nchini, COTU, Francis Atwoli wakiwataka wauguzi hao waliheshimu agizo la Rais na kurejea kazini.

Kwenye Kaunti ya Embu, wauguzi hao wamesema vitisho vya Rais Kenyatta kwamba  watakaokiuka agizo lake watasimamishwa kazi si suluhu ya matatizo yanayowakabili.

Wakiongozwa na Katibu wao kwenye Kaunti ya Embu, wauguzi hao wamesema wanachotaka kitimizwe ni mkataba wa malipo baina yao na serikali ya kaunti sawa na inavyofanyika kwenye kaunti nyingine ambazo hakuna mgomo.

Katibu huyo aidha amesema agizo la Rais Kenyatta limechangia kusambaratika kwa hatua zilizopigwa kati yao na serikali ya kaunti ili kutafuta suluhu.

Hali sawa na hiyo inashuhudiwa kwenye Kaunti ya Taita Taveta huku wauguzi wanaogoma katika Hospitali ya Rufaa ya Moi wakiwa bado hawajarejea kazini.

Aidha kulingana na mmoja wauguzi katika Hospitali ya Kitaifa ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya uti wa mgongo, Rais alishauriwa visivyo kuhusu chanzo cha mgomo wa wauguzi.

Hata hivyo kwenye Kaunti ya Trans Nzoia, udadisi wa Radio Maisha umebaini kuwa baadhi ya wauguzi ambao hawajavalia sare rasmi za kazi wamerejea japo hawawahudumii wagonjwa. Hizi hapa kauli za baadhi ya wagonjwa ambao wamelazimika kuondoka katika Hospitali ya Level mjini Kitale ilio kutafuta huduma za matibabu katika vituo vya afya vya binafsi.

 
Hayo yanajiri huku Waziri wa Leba, Ukur Yatani akiwataka wauguzi kuliheshimu agizo la Rais Kenyatta na kurejea kazini mara moja. Akiwahutubia wanahabari jijini Nairobi, Yatani amesema agizo hilo linaambatana na lile lililotolewa na mahakama kwamba wasitishe mgomo na kuruhusu mazungumzo.

Yatani amesema huenda serikali za kaunti vilevile serikali ya kitaifa zikalazimika kuwaadhibu wauguzi ambao hawatarejea kazini kwani watakuwa wakigoma kinyume na sheria. Aidha amesema kamati maalum iliyobuniwa kutafuta mwafaka kuhusu matatizo yanayowakabili wauguzi leo hii itafanya vikao zaidi na Tume ya Kuratibu Mishahara ya Wafanyakazi wa Umma, SRC ili kufanya mashauriano zaidi.

Wakati uo huo, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU Francis Atwoli amewataka wauguzi hao kurejea kazini. Japo amesema wana haki kisheria kugoma, amewashauri kuipa kamati maalum ya upatanisho nafasi ya mazungumzo kutafuta mwafaka. Amerejelea kauli yake kwamba Wizara ya Leba ina jukumu la kuushughulikia mgomo huo na haina haja ya kumhusisha rais.

Wakati uo huo, amemkosoa Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Wycliff Oparanya kwa kutoa vitisho kwa wauguzi na badala yake kufuata mkondo wa kisheria, kama vile kukubali mkataba wa utendakazi huku akimshtumu Waziri Yatani kwa madai ya kutokuwa na uwezo wa kuisimamia Wizara ya Leba na kusema iwapo angekuwa, Rais angekuwa ashamfuta kazi.

Je, kisheria wauguzi na viongozi wao wanaweza kuchukuliwa hatua zozote kwa kukiuka agizo la mahakama na lile la Rais? Wakili Dancan Okach anasema kwanza kabisa Rais Kenyatta alikuka sheria kwa kutoa agizo jingine kwa wauguzi kwani tayari mahakama ilikuwa imetoa agizo hilo na lilistahili kuheshimwa mara moja.

Okach anasema bodi za uajiri za kaunti ndizo zenye mamlaka ya kuwachukulia hatua wauguzi ambao hawajarejea kazini na utaratibu wa kisheria unastahili kufuatwa kwa kuwasilisha kesi ya kulalamikia kukiukwa kwa maagizo ya mahakama. Wakili huyo anasema licha ya kwamba serikali ya kitaifa ndiyo hutoa mgao wa fedha kwa serikali za kaunti ili kuendesha shughuli zake, haina mamlaka ya kufanya maamuzi kuhusu namna shughuli zinavyoendeshwa kwenye kautni hizo.

Hapo kesho pande zote zinazohusika zitafanya kikao cha pamoja katika Wizara ya Leba kujadiliana yaliyoafikiwa kabla ya kutoa mwongozo zaidi.