Waliowatupa ''Chokoraa'' msituni kuadhibiwa; asema Gavana Kinyanjui

Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui ameapa kuwa waliowatupa watu 41 msituni kaunti ya Baringo wataadhibiwa.

Hayo yanajiri huku jumla ya watoto thelathini na sita miongoni mwa watu arubaini na mmoja wa kurandaranda mitaani kwenye Kaunti ya Nakuru waliotupwa katika msitu wa Chemusus ulioko Kaunti ya Baringo, wamerejeshwa. Maafisa wa usalama wakiongozwa na msirikishi wa utawala wa Kuanti ndogo ya Eldama Ravine David Aenga amesema wote wameondolewa msituni. Inaarifiwa miongoni mwa waliorejeshwa kuna jumla ya watoto kumi na wawili walio chini ya umri wa miaka kumi na minane na tayari wamehojiwa ili kuwasaidia polisi katika uchunguzi.


Wakati uo huo, serikali Kaunti ya Nakuru imeshtumiwaa vikali kwa kuwatupa msituni jumla ya watu arubaini na mmoja wa kurandaranda mitaani. Wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Naivasha, John Mututho, amesema lengo la usimamizi wa Kaunti ya Nakuru lilikuwa kuwaua, huku akitoa wito kwa uchunguzi kufanywa na waliohusika wachukuliwe hatua.
Kwa upande wake, mmoja wa wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kwenya Kaunti ya Nakuru Simon Ole Nasieku, amesema Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui, anastahili kuchunguzwa kufuatia suala hilo.


Alhamisi watu hao wa kati ya umri wa miaka kumi na miwili na ishirini na sita walipatikana katika msitu wa Chemusus Kuanti ya Baringo. Waliwaeleza maafisa wa polisi kuwa maafisa wa serikali ya Kaunti ya Nakuru waliwahadaa kwamba walikuwa wakiwapelekwa shuleni ila wakawatupa msituni Jumatano usiku.