Mahakama yaendelea kulaumiwa kwa kulemaza vita dhidi ya ufisadi

Inasubiriwa kuona iwapo idara ya mahakama itabadili mtindo wake wa kuwaachilia kwa dhamana washukiwa wakuu wa ufisadi baada ya vitengo mbalimbali vya serikali kuilaumu idara hiyo kwa kulemaza vita dhidi ya ufisadi kupitia maamuzi mbalimbali inayofanya ya kuwaachilia kwa dhamama washukiwa. Akihutubu wakati wa kongamano la kukabili ufisadi jijini Nairobi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Paul Kihara alisema baadhi ya maamuzi ambayo yamekuwa yakifanya na mahakama ni ya kustaajabisha.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Upelelezi, DCI George Kinoti ambaye alisema kuwa maagizo mengine yakuzipinga kesi mbalimbali yamekuwa yakitolewa hata kabla ya kesi zenyewe kupiga hatua kubwa.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP Noordin Haji aidha alisisitiza haja ya kujiondoa ofisini kwa baadhi ya washukiwa wanaohusishwa na kesi mbalimbali kwani ndiyo hatua wanayostahili kuchukua kisheria.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC Twalib Mbarak vilevile alilalamikia kuendelea kujigamba kwa baadhi ya washukiwa kwamba wanatekeleza majukumu yao kulingana na sheria ilhali wananchi wanaumia chini ya uongozi wao.

Hivi majuzi Jaji Mkuu, David Maraga kwa upande wake aliishtumu ofisi ya DPP na ile ya DCI kwa madai ya kuwasilisha mahakamani kesi zisizo na uzito hali ambayo imekuwa ikichangia kutupiliwa mbali kwa kesi hizo.

Related Topics

Maraga ufisadi