Rais Kenyatta afanya uteuzi serikalini

Rais Uhuru Kenyatta amefanya uteuzi mpya serikalini ambapo amemteua aliyekuwa Spika wa Seneti, Ekwe Ethuro kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, HELB wadhifa atakaoushikilia kwa kipindi cha miaka 5. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, IEBC Isaack Hassan ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Viwanda.

Mjane wa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Uchaguzi, IEBC Chris Musando, Eva Buyu Musando aidha ameteuliwa kuwa mwanachama wa Mamlaka ya kushughulikia usafirishaji wa bidhaa hadi mataifa ya nje. Ameteuliwa pamoja na Kisoi Munyao na John Masaba. Aliyekuwa Seneta wa Kitui, David Musila ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Makavazi ya Kitaifa.

Aliyekuwa mwaniaji ugavana kwenye Kaunti ya Uasin Gishu, Zedekhaih Bundotich maarufu Buzeki kuwa Mwenyekiti wa bodi ya Kampuni ya Sukari ya Chemilil. Anatarajiwa kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitatu katika wadhifa huo. Ikumbukwe Buzeki alishindwa na Jackson Mandago katika kinyang'anyiro cha ugavana.

Aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Muungano wa NASA, Norman Magaya ameteuliwa pamoja na watu wengine wanne kuwa wanachama wa Bodi ya Filamu nchini kwa kipindi cha miakam mitatu. Aidha Moses Akaranga ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Hazina ya Mazingira.  Wengine walioteuliwa kwa nyadhifa mbalimbali ni Thomas Mwadeghu, Yusuf Chanzu.

Related Topics

Uhuru uteuzi