Ibada ya wafu ya waliofariki dunia Solai yafanyika

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto leo hii wamehudhuria ibada ya watu 47 walioaga dunia katika mkasa wa Solai, Nakuru. Rais Kenyatta ameahidi kuzipa familia zilizoathirika usaidizi unaohitajika ili kuanza maisha yao upya. Wito wa kuwekwa kwa mikakati ya kukabili majanga vilevile ulishamiri wakati wa ibada hiyo.

Ni ibada ya wafu iliyowaleta pamoja watu wa matabaka mbalimbali katika Kanisa la AIC, Solai Kaunti ya Nakuru kuwapa buriani walioaga dunia kufuatia kusombwa na maji ya Bwawa la Patel wiki iliyopita. Rais Uhuru Kenyatta aliyefika kuomboleza na waathiriwa akiahidi kutoa usaidizi unaohitajika kwa waathiriwa akisema serikali itagharimia ujenzi wa shule zilizosombwa, vilevile kurekebisha huduma za nguvu za umeme ambazo zilikatizwa wakati wa mkasa huo.

Rais Kenyatta aidha ameagiza kwamba wote walioathiriwa na mafuriko kwenye maeneo mbalimbali nchini wasajiliwe katika Bima ya Kitaifa ya Huduma za Afya, NHIF ili kuwapunguzia gharama za kutafuta huduma za matibabu.

Naibu wa Rais, Willliam Ruto kwa upande wake amesema si wakati wa kulaumiana kuhusu ni nani aliyechangia mkasa huo wa Solai, ila ni wakati wa kutafuta suluhu. Aidha amesema mpango wa kutoa hati-miliki za ardhi kwa wakazi wa eneo la Nyakinywa Nakuru, inaendelea.

Kwa upande wake, Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui ameisihi serikali kutozisahau familia zilizoathirika, huku akimpongeza mhudumu wa kliniki moja kwa jina Mary Warughuru kwa kuchangia pakubwa kuwaokoa waathiriwa wa mkasa huo.

Awali shughuli ya kuichukua baadhi ya mili ya walioaga kufuatia mkasa huo ilifanyika katika Hifadhi ya Hospitali ya Nakuru. Ikumbukwe wengi wa walioaga dunia ni wanawake na watoto. Kulingana na Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu, Abbas Gullet, walioaga dunia katika mkasa huo wametambuliwa, isipokuwa mmoja.

Aidha amesema kwa kipindi cha siku chache zijazo, waathiriwa watapewa fidia ya kuanzia shilingi elfu thelathini huku baadhi wakikabidhiwa vitambulisho vipya vya kitaifa, kwa vile walivyokuwa navyo vilisombwa na mafuriko. Baadhi ya mili inatarajiwa kuzikwa punde baada ya hafla ya leo huku baadhi ya familia zikisema zitawazika wapendwa wao, katika kaburi la pamoja. 

Related Topics