Usajili kuendelea hadi Februari 19

Na, Beatrice Maganga
Shughuli ya kuwasajili wapigakura wapya itaendelea kote nchini kufuatia amri ya mahakama kwamba shughuli hiyo iendelee hadi siku ya Jumapili wiki hii. Akitoa uamuzi huo jana, Jaji wa Mahakama Kuu, Chacha Mwita alisema hatua hiyo itatoa fursa ya kusajiliwa kwa wananchi ambao hawajafanya hivyo.

Jaji Mwita alisema usajili unaoendelea sasa ni wa halaiki japo Tume ya Uchaguzi, IEBC imedhihirisha kwamba huenda shughuli hiyo ikaendeshwa kwa njia tofauti hadi kufikia Mei 17, miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu.
Kesi ya kutaka kuongezwa kwa muda wa usajili ilikuwa imewasilishwa na Mwanaharakati Okiya Omutata kwa misingi kwamba Wakenya ambao vitambulisho vyao vya kitaifa vilicheleweshwa huenda wangefungiwa nje iwapo shughuli hiyo ingekamilika Februari 14 jinsi ilivyoratibiwa awali.

Wakili  wa IEBC Erick Gumbo alisema japo kuna uwezekano wa usajili kuendelea katika ofisi za tume, gharama za kuendesha shughuli hiyo zitaongezeka na huenda tume ikalazimika kuliomba bunge kuongeza bajeti yake. Kuongezwa kwa muda wa usajili wa halaiki kunatarajiwa kuigharimu tume kima cha shilingi milioni 210.
Ikumbukwe usajili katika magereza 118 humu nchini vilevile umeratibiwa kuanza Februari 20 hadi 27.

Related Topics

IEBC Chacha Mwita