Mvutano wachacha bungeni kuhusu VAT

Hatimaye Spika wa Bunge la Kitaifa, Justine Muturi ametangaza kuidhinishwa kwa mapendekezo ya Rais Uhuru Kenyatta ya kupunguza thamani ya kodi ya ziada kutoka asilimia 16 hadi asilimia 8 licha ya pingamizi kutoka kwa wabunge kuhusu namna shughuli ya kupiga kura ilivyoendeshwa. Kikao cha kujadili marekebisho hayo kilishamiri vurumai wakati wabunge walipoangizwa kupiga kura kwa mara nyingine licha ya awali kuangusha mapendekezo ya Rais. Aidha Kiongozi wa Wengi katika bunge hilo, Adan Duale na mwenzake wa Wachache, John Mbadi walizomewa na wabunge huku wakishtumiwa kwa madai ya kuwachochea wabunge wengine kuondoka katika majengo ya bunge ili wasifikishe idadi inayohitajika ya kuangusha mapendekezo ya Rais.

Ndivyo hali ilivyokuwa baada ya Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Narok, Soipan Tuya kutangaza kwamba idadi ya wabunge waliokuwa katika majengo ya bunge ilikuwa 215, ilhali idadi inayohitajika ni wabunge 233, hivyo kupita kwa mswada wa marekebisho yaliyopendekezwa na Rais kwa mujibu wa sheria za bunge.  Awali kura ilipopigwa, upande wa wanaopinga uliibuka mshindi katika kura hiyo.

Baadhi ya wabunge walipinga kauli kwamba haikuwapo idadi ya kutosha ya wabunge huku wakiibua madai kwamba Duale na Mbadi waliwaagiza wabunge wengine kuondoka wakati makarani wa bunge walipotakiwa kuhesabu idadi ya wabunge.

Ikamlazimu Spika Justine Muturi kuwaagiza wabunge watano wa kila upande kuwasilisha malalamishi yao kuhusu kura hiyo. Wote waliozungumza wakasema wakati wa awamu ya kwanza ya upigaji kura, ilikuwa bayana kwamba marekebisho hayo yalikuwa yameangushwa na bunge. Wabunge  TJ Kajwang, Millie Odhiambo, Mohammed Ali Gathoni wa Muchomba na Mwakilishi wa Kike, Cathrine Waruguru ni miongoni mwa waliolalamika.

Spika Justine Muturi vilevile alieleza kushangazwa na kasoro zilizoshuhudiwa katika tarakilishi za bunge ambazo zilionesha kwamba idadi ya wabunge waliokuwamo ilizidi idadi jumla ya wabunge.

Ilimlazimu Spika Muturi kusitisha vikao hivyo kwa muda wa dakika kumi na tano ili kukiruhusu kitengo cha teknolojia katika bunge kurekebisha dosari zilizoshuhudiwa kuhusu idadi ya wabunge kabla ya kikao kuendelea.

Aliporeja Muturi alitoa amri ya kuidhinisha mapendekezo hayo huku wabunge wakimzomea na kuimba Wimbo wa Bado Mapambano kudhihirisha kutoridhishwa na uamuzi huo wa Spika huku wakishinikiza kodi hiyo ipunguzwe hadi sufuri.

Katika kikao cha asubuhi, bunge lilidhinisha kupunguzwa kwa bajeti ya ziada ya mwaka wa kifedha wa 2018/ 2019 kwa kima cha shilingi bilioni 37.6 kwa ujumla. Miongoni mwa fedha zilizopunguzwa ni zile za kuendeleza huduma za Mawasiliano na Teknolojia, ICT fedha za miradi ya barabara, zile za ununuaji wa vipakatalishi kwa wanafunzi wa shule za msingi miongoni mwa nyingine.

Fedha za kutekeleza miradi inayosimamiwa na wawakilishi wa kike zimepunguzwa kwa kima cha shilingi milioni 200 huku zile za CDF zikipunguzwa kutoka shilingi bilioni 35 hadi shilingi bilioni 33. Hata hivyo fedha za idara ya mahakama zimeongezwa kwa shilingi bilioni 1.5 zaidi.  

Related Topics

Uhuru Muturi