Mwanasheria Mkuu akanusha madai ya kupotea kwa faili kwenye sakata ya ufisadi katika wizara ya afya

Na Carren Omae na Mike Nyagwoka

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekanusha taarifa kuwa faili za kampuni zilizopokezwa zabuni na Wizara ya afya zimetoweka.Kitengo cha haki katika ofisi hiyo kimesema kuwa stababadhi zote za kampuni zipo kwenye faili na hata kwenye sajili ya eletroniki. Vilevile ofisi hiyo imesema wakenya wanaruhuisiwa kuzikagua faili hizo.
Ikumbukwe madai yaliibuliwa kuwa wafanyakazi wa ofisi walikuwa wameshindwa kupata faili za kampuni ya Uwekezaji ya Estama, iliyosajiliwa kama EPZ, na Maisha Care Medics. Kampuni hizo mbili zinadaiwa kupokea pesa zilizotengwa kwa ajili ya wagonjwa, akina mama wajawazito na watoto wanaozaliwa.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa EACC Michael Mubea alisema Tume hiyo kwa ushirikiano na Wizara ya afya zimebuni jopo litakalochunguza madai hayo. Jopo hilo litatakiwa kuwasilisha ripoti yake kwa kipindi cha siku 30 zijazo.

Kulingana na Mubea Wizara hiyo imeahidi kushirikiana nao katika uchunguzi huo.

Ameyasema hayo baada ya maafisa wa EACC kuvamia ofisi za Wizara ya Afya  kutafuta stakabadhi muhimu kusaidia katika uchunguzi.