Serikali yatoa marufuku ya kutotoka nje Mandera

Na Carren Omae na Frederick Muitiriri

Kufuatia shambulio katika Kaunti ya Mandera siku ya Jumanne ambapo jumla ya watu kumi na wawili waliuliwa, serikali imetangaza Marufuku ya kutotoka nje eneo hilo. Waziri wa Masula ya Ndani ya Nchi, Joseph Nkaiserry amesema wakazi hawatatakIwa kutoka nje kuanzia saa kumi na mbili unusu jioni hadi saa kumi na mbili unusu asubuhi katika kipindi cha miezi miwili kuanzia leo hii hadi Disemba 27.
Maeneo yatakayoathirika na marufuku hayo ni Mandera Mjini, Omar Jillo, Arabia, Fino, Lafey Kotulo, Elwak na maeneo yaliyo umbali wa kilomita ishirini kutoka mpaka wa Kenya na Somalia.
Wakati uo huo, Mahakama ya Mandera imewaruhusu maafisa wa polisi wa kitengo cha kukabili ugaidi, ATPU kumzulia mlinzi Abdirahman Ali wa Hoteli ya Baasharo kwa siku kumi. Kulingana na maafisa wa polisi, Abdirahman Ali mwenye umri wa miaka ishirini na mmoja anashukiwa kuwasaidia magaidi hao kutekeleza shambulio hilo. Inadaiwa kwamba hakulala katika hoteli hiyo usiku wa shambulio ilivyo kawaida. Inasemekana kwamba usiku huo, alilala katika jengo tofauti lililo umbali wa mita 15 kutoka hoteli hiyo. Aidha anashtumiwa kwa kutoripoti kisa hicho suala ambalo amelipinga.
Mahakama imekubali ombi la maafisa wa polisi ikisema uchunguzi zaidi lazima ufanywe ili kuzuia mashambulio zaidi. Kesi hiyo itasikilizwa tarehe 7 mwezi ujao.