Tuzo za KUMIKUMI zilinoga!

Na Hassan Ali
    Ni kiungo kidogo sana! Kiungo ambacho hugeuza shubiri ikawa tamu; na asali kuwa chungu! Ulimi ambao kwamba watangazaji hutumia wawapo hewani. Na hapo wakairemba na kuitia nakshi lugha na kufaulisha mawasiliano au ulimu huo ukachafua lugha na kuitia najsi kama afanyavyo lipyoto!
    Labda hapo ulipo wajiuliza ULIMI na KUMIKUMI ni nini?
    Mwalimu-mtafiti-mwandishi-malenga-nguli, maarufu na mahiri Wallah bin Wallah, kaandika saaana. Kafunza kwiingi! Kahangaikia mno Kiswahili. Na wasemavyo cha jasho hakikosi utamu.
    Alichumia juani na sasa yualia kivulini. Katokwa jasho kwapani akikimbizana na Kiswahilli, leo hii yeye sio kwamba tu anachangia mno makuzi na maenezi ya lugha ya Kiswahili kupitia vitabu na vyombo vya habari, lakini pia kwake nyumbani, WASTA VILLA, eneo la Matassia (Ngong) viungani mwa jiji la Nairobi. Mwalimu huyu mtajika kajenga ukumbi na maktaba ya wasomi, walimu, wanafunzi wa lugha kwenda kusoma, kufanya utafiti na kuhoji kuhusu Kiswahili.
    Ili kuwafikia wapenzi wa lugha walioko nje ya mipaka ya Kenya, kituo hicho cha Kiswahili, kikaasisi hafla maalum, sherehe mzo, tuzo ziitwazo KUMIKUMI. Kila mwaka, tarehe KUMI mwezi wa KUMI, shajara na kalenda ya Waswahili kote ulimwenguni kuna asteriski ya KUMI KUMI.
Lengo na madhumuni kuwatuza ‘wangali hai’ wanahabari, walimu, waandishi, wanafunzi na wapenzi wote wa lugha ashirafu ya Kiswahili. Huo ulikuwa mwaka 2010, mwezi OKTOBA tarehe KUMI. Ndio usuli na asili ya UTATU wa KUMIKUMI.
    Mwaka huu, kunako tarehe kumi mwezi Oktoba, ziliandaliwa tuzo hizo za KUMIKUMI makala ya saba. Na zilinoga kweli. Zilifaulu hadi!
    Kama mwaka jana, makala ya mwaka huu yalivutia idadi kubwa ya wapenzi wa Kiswahili na ukumbi ulijaa pomoni. Ulitapika! Usisahau sherehe za mwaka huu zilifanyika siku ya JUMATATU. Si wikiendi. Wapo walionyimwa udhuru wakavunja miko ya kwahali kwao kwa kazi! Walii huvunja kanuni ati!
    Mwalimu Wallah bin Wallah na mwanahabari mkongwe aliyewahi kufanya kazi na mashirika ya DW, BBC na sasa ni mhariri wa habari za michezo shirika la AZAM, Charles Hillary Martin, waliwaasa wanahabari kufanya tahadhari sana wawapo hewani hasa matumizi ya lugha. Ndio hapo nakurejesha juu mwanzoni mwa makala haya: Kiungo hiki ulimi.
    Profesa Malonga alipopanda jukwaani kuelezea ni kwa vipi Kiswahili kinavyokua na kuzagaa nchini kwao Rwanda na nchi nyinginezo za ukanda huu kama Burundi, Uganda, Sudan Kusini na kwingineko, sote ukumbini tulipandwa na jazba. Madadi hasa!
    Dk. Musa Hans akasimulia ya kwao Tanzania hasa vyuoni, vyombo vya habari na CHAKAMA. Aligusa nyoyo za wengi.
    Hafla ya mwaka huu ilitumiwa pia kuzindua vitabu viwili na wandishi wavyo walikuwepo kutia sahihi kwa wanunuzi. MASHATENI WAMERUDI (Prof. S.A Mohammed) na VIFARU WEUSI (Dk. M.S. Khatib).
    Mwanahabari na malenga hodari Nuhu Zuberi Bakari aliwaongoza malenga wengineo kutoa tumbuizo za mashairi. Wacha tu! Mashairi yangali yanarindima akilini mwangu. Hadi mwakani tena OKTOBA KUMI panapo uhai…mbona naona MBALI SANA!
    Ulikuwa mlahaka wa Kiswahili na Waswahili usiokuwa na kifani. Chambilecho mshairi na mwanamuziki kutoka Bongo Mrisho Mpoto: “Sherehe zilikuwa TAMU kama NINI!!!”
Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA).
[email protected], [email protected],
FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali,
Twitter: @alikauleni