Laboso asema kipengee cha kuwazuia wanasiasa kuhama vyama kilikuwa kandamizi

Na, Beatrice Maganga

Baada ya kusitishwa jana, hatimaye Bunge la Kitaifa limerejelea mjadala kuhusu ripoti ya Kamati ya Pamoja iliyojadili hatma ya makamishna wa Tume ya Uchaguzi, IEBC na mfumo wa uchaguzi kwa ujumla, baada ya Naibu Spika Joyce Laboso kuidhinisha marekebisho kwenye kipengele ambacho kingewazuia wanasiasa kuvihama vyama vyao wanaposhindwa katika uteuzi wa kuwania nyadhifa mbalimbali.
Akitoa uamuzi huo kwenye kikao cha alasiri, Laboso amesema kipengee hicho kinakiuka haki za wawaniaji wa viti mbalimbali vya kisiasa.Hata hivyo amewashauri wabunge kutafuta ushauri wa viongozi wao iwapo wanahitaji mabadiliko zaidi ikizingatiwa kuwa ripoti hiyo iliandaliwa na wajumbe wa CORD na Jubilee.
Licha ya kuunga mkono ripoti hiyo baada ya kufanyiwa marekebisho, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Adan Duale amesema hulka ya kuhama vyama ni mtindo usiyofaa. Kiongozi wa Wachache katika bunge hilo, Francis Nyenze kwa upande wake ameuunga mkono uamuzi huo wa spika akisema ni wa busara. Wabugne wengine aidha wamedai kwamba huenda watu waliokijumuisha kipengele cha kuzuia kuhama kutoka kwa chama kimoja hadi kingine walikuwa na njama fiche.
Awali Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa CORD Raila Odinga waliipitisha ripoti hiyo iliyoandaliwa na Kamati iliyoongozwa na maseneta, James Orengo na Kiraitu Murungi jinsi ilivyo. Seneti vilevile ilidhinisha ripoti hiyo jana bila kuifanyia mabadiliko.

 

Related Topics