Ghasia zashuhudiwa katika uchaguzi mdogo Nyacheki

Na Sammy Omingo

Wakazi wa Wadi ya Nyacheki Eneo Bunge la Bobasi Kaunti ya Kisii, Jumatano wamefanya uchaguzi mdogo huku visa vya kuhongwa kwa wapigakura vikiripotiwa. Ghasia zilishuhudiwa katika kituo cha Mochengo wakati Mwakilishi wa Wadi ya Bogetorio, Bonny Okenye aliposhutumiwa na vijana waliokuwa na hasira kwa ununuzi wa kura katika kituo hicho hali ambayo ilisababisha Okenye kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya vijana hao.

OCPD wa Nyamache Japhet Murichia amesema uchunguzi umeanzishwa na iwapo mwakilishi huyo atapatikana na hatia atakamatwa ili kubaini iwapo anamiliki bunduki hiyo kisheria. Hata hivyo Murichia amemsihi yeyote aliye na habari kuhusu wanaowahonga wapigakura kuripoti visa hivyo katika ofisi yake ili uchunguzi uanzishwe.
Afisa wa Tume ya Uchaguzi IEBC eneo hilo, Jackiline Osiemo amewasihi wapigakura kutobaki katika vituo vya kupiga kura baada ya shughuli hiyo ili kuwapa wakati maafisa wake kuendesha shughuli hiyo bila matatizo.

Awali afisa mmoja wa chama cha Jubilee alitimuliwa na vijana wenye hasira kwa tuhuma za kuwahonga wapigakura, huku maafisa wa polisi wakilazimika kumwokoa mmoja wa wanasiasa Abaga Sagero ambaye vilevile anatuhumiwa kwa ununuaji wa kura.
Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya kifo cha Peter Nyaega aliyeaga dunia Julai 25 mwaka huu baada ya kuugua, na kimewavutia wawaniaji kumi na watano.