Makamanda wahamishwa

Na Sophia Chinyezi

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Elgeyo Marakwet Sharif Abdallah amehamishwa kufuatia mapigano baina ya jamii hasimu ambayo yamesababisha vifo vya watu sita na wengine kuachwa bila makao. Kamanda mpya wa polisi eneo hilo ni Tom Odera wa Kajiado.

Abdallah amehamishwa hadi Nairobi kuwa Mkuu wa Oparesheni. Kipkemoi Rop kutoka Taita ndiye Kamanda mpya wa Kaunti ya Kajiado, huku OCPD wa Keiyo Kaskazini Fredrick Ochieng akipandishwa cheo na kuwa Mkuu wa Polisi Kaunti ya Taita Taveta.

Patrick Mwakio vilevile amehamishwa kutoka Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Kiganjo hadi makao makuu ya Tume ya Huduma za Polisi NPSC, Idara ya Mipango.
Mabadiliko hayo yametangazwa katika makao makuu ya polisi jijini Nairobi. Kamishna wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Fredrick Ndambuki anasema mapigano hayo yalikuwa baina ya jamii za Kapsiren na Kapshoi.