Mvutano wazidi kushuhudiwa katika tume ya EACC

Na, Sophia Chinyezi

Tofauti zinaendelea kuibuka kuhusiana na hoja zilizowasilishwa na mwanaharakati mmoja kuhusu kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC, Phillip Kinisu. Kinisu anachunguzwa kufuatia madai kwamba kampuni yake ya Esaki ililipwa zaidi ya shilingi milioni thelathini na tano kupeleka vifaa vya kuchimba kisima katika Taasisi ya Taifa ya Huduma za Vijana NYS, kati ya mwezi Oktoba 2014 na Novemba 2015.

Mapema leo Kamishna wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC, Rose Mgoi Macharia aliwasilisha kesi mahakamani kupinga hoja zilizowasilishwa na Okiya Omtata, akimlaumu kwa kuhusika na mikakati ya kumng'atua mamlakani Kinisu. Macharia amesema ombi la Omtata halina msingi, hivyo linastahili kutupiliwa mbali. Katika kesi aliyoiwasilisha katika Mahakama ya Milimani, Macharia amesema mahakama haina mamlaka kisheria kusikiliza na kuamua ombi la Omtata.

Omtata anataka Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Michael Mubea na Kamishna Macharia kushirikishwa katika kesi yake akisema hatua hiyo itasaidia kuithibitishia mahakama kwamba matatizo yanayoshuhudiwa katika EACC yanachangiwa na wawili hao.