×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Moha Jicho Pevu: Hotuba ya Uhuru kwa vibaraka wa Jubilee

County_Nairobi
  
 President Uhuru Kenyatta

Waswahili hawakukaanga mbuyu waliponena kuwa mimba ya mwana haramu, huingia mara ya kwanza na ya pili, ni kusudi.

Ukweli wa msemo huu ulionekana wazi pale Rais Uhuru Kenyatta alipotoa hotuba yake kwa taifa juma lililopita.

Rais Uhuru aliingia bungeni kwa mahanjam huku ‘maskauti 36’, almaaruf ‘The 36 beggars’ wakimpigia debe na kujaribu kufananisha hafla hiyo na ile ya Rais wa Marekani Barrack Obama.

Wakenya waliolemazwa na kufanywa watumwa ndani ya taifa lao walikuwa na matumaini ya kusikia mapya kutoka kwake rais Uhuru.

Wakenya walikuwa na matumaini kuwa masuala ya ufisadi, ajira kwa vijana na afya yangepewa kipau mbele katika hotuba hiyo. Wengi walitarajia rais kuwachukulia hatua kali za kisheria mafisadi wote serikalini. 

Na hata kabla ya hotuba hiyo kuanza upande wa upinzani walitoa lalama zao kwa kusitisha hotuba hiyo kwa kupiga firimbi.

Uhuru Kenyatta alidhalilishwa na kupewa ujumbe kuwa wakenya wamechoka na uongozi wake uliojawa na ukabila, ufisadi na dhulma.

Baada ya spika wa bunge la Jubilee samahani, spika wa bunge la wabunge wa serikali, samahani tena, spika wa bunge la Kenya kutumia sheria za ghushi kuwatupa nje wabunge kwa kuwaita kwa majina yao, wabunge wa Jubilee walianza kuvumbua majina ya kiajabu.

Kwa mafano walitangaza kuwa wabunge waliozua kero walikuwa wabunge wajaluo, mara wabunge wa Cord, watu wasiotahiriwa, wajinga, watoto na kadhalika.

Wale maskauti 36 pia walianza kuimba nyimbo za miungu yao midogo midogo na kupakaza chuki na ukabila zaidi. Walichosahau ni kuwa Simba Arati sio mjaluo, Bosire pia sio Mjaluo.

Wale wote waliopiga firimbi ni wakenya kwanza. Wana Jubilee walisahau kuwa mkuki kwa nguruwe ni mtamu kwa binadamu kali.

Miaka ya nyuma, enzi za uongozi wa Rais mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi, hususan mwaka wa 1978, wabunge waliojiita ‘The Agikuyu Mps’ chini ya uongozi wa MJ Kariuki na Njenga Karume, walimfokea rais Moi na kupiga firimbi kabla ya kutoka nje ya majengo ya bunge.

Mwaka wa 1993, viongozi kutoka Gema wakiongozwa na Kenneth Stanley Njindo Matiba, George Nyanja miongoni mwa wabunge wengine arobaine, vile vile walimkemea Moi wakiwa wameshika mabango na kupiga kelele ndani ya bunge kabla ya kuondoka.

Viongozi hawa walionekana kama mashujaa kwa kusimama na kupinga uongozi wa Moi. Wabunge hao walisifiwa sana kwa sababu labda waliyekuwa wakipinga alikuwa Mkalenjin ambaye hawakutarajia kuwaongoza baada ya kifo cha Hayati Jomo Kenyatta.

Wengi waliona uongozi wa Moi kama mawingu yanayopita. Zamu ya Uhuru Kenyatta imefika na sasa kwa sababu rais sio Mkalenjin, bali ni mmoja wao, sasa hili linaonekana kuwa kero na utoto.

Hili linawachoma kwa sababu ni zamu ya mwenzao kuoshwa na maji ya kunde.

Hii ndio Kenya ya sasa. Kenya ya kudanganyana na kupakana siagi. Sasa viongozi wa jubilee wanajifanya weupe kama pamba. Martha Karua alipojiondoa katika mkutano wa Rais mtaafu Daniel Moi alionekana kama shujaa na bingwa lakini ikifika zamu ya mmoja wao, basi wote kwa pamoja wakiwemo wafuasi wao, wanapewa majina ya kimaajabu kando na kutusiwa. Seneta wa Nairobi Gideon Mbuvi alirekodiwa akisema kuwa atapendekeza IEBC kabla ya kutoa idhibati kwa mwanasiasa yeyote ambaye lazima awe ametahiriwa.

Sonko alimdhalilisha Mbunge wa mbita Millie Odhiambo kwa kusema kuwa watamtafutia dume limzime makali yake. Hawa ndio viongozi wenyu wakenya. Katika serikali hii ya Uhuru Kenyatta ukitaka kuwa maarufu kuwa mwizi nambari moja. Utapendwa na kusifiwa na wezi wenzako. Pia huwe mkabila nambari moja kwani utasifiwa na kabila lako.Hii ndio demokrasia ya Kenya.

Tukirudi katika hotuba ya Uhuru Kenyatta, ukweli wa mambo ni kwamba lau kama angelifanya hotuba yake katika bustani la uhuru park, basi firimbi zingelizidi kupigwa na wakenya waliochoka na uongozi wake, spika wa bunge angelitia akili siku hiyo kwani wakenya wangemwachia uwanja huo yeye, Uhuru Kenyatta na wabunge wa jubilee wafanye wapendavyo.

Iwapo ningekuwa Rais Uhuru, ingawa singelipenda kujipa mfano huo, ningejiuliza masuali chungu nzima. Kwanza ningejiuliza ni kwa nini wakenya hawanipendi? Ni kwa nini wakenya wamepoteza imani nami? Ni kwa nini nimeshindwa kutatua shida za wakenya? Ni kwa nini waajiriwa wangu wanaibia wakenya kila kukicha? Na hatimaye nani ndiye Rais wa Kenya kiasi cha kuwaachilia wafisadi kubaka taifa!

Kumbuka hii ilikuwa nafasi ya mwisho kwa rais Uhuru kuweka mambo sawa. Hamna nafasi nyengine ya kuwaunganisha wakenya, ewe rais. Viongozi wa Jubilee sasa wanataka tutahiriwe mara ya pili, viongozi wa Jubilee wanatutusi sisi wapiga kura na kabila zetu. Lakini kabla kututahiri sisi wakenya walalahoi, hebu mtahiri sio sehemu zenu za siri.

Kumbuka Mungu hana kabila wala chama. Ewe rais usiwafurahie wezi wanaoiba ndani ya serikali yako, na kukufanya wewe uonekane ovyo. Umeshatia msumari wa mwisho katika jeneza la wakenya, lililosalia ni wao kukataa kuzikwa kwa lazima wakiwa hai kwa kuvunja jeneza hilo na kukomboa uhuru wao mwaka wa 2017.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles