Jubilee yataka IEBC kuondoka kwa hiari

NA ,FREDRICK MUITIRIRI

Jubilee yataka IEBC kuondoka kwa hiari

Mrengo wa Jubilee umetangaza kwamba unaunga mkono suala la makamishna wa Tume ya Uchaguzi nchini IEBC kuondoka ofisini. Aidha mrengo huo umependekeza makamishna hao wajiondoe ofisini kwa hiari. Wakizungumza mbele ya kamati ya pamoja inayojadili hatima ya makamishna wa tume hiyo, muungano huo umesema hatua hiyo imechukuliwa kwa kuzingatia kuwa huenda kukawa na marudio ya upigaji kura wakati wa uchaguzi mkuu ujao na muda wa makamishna hao utakuwa umekamilika.
Muungano huo umepinga mapendekezo ya makamishna kutolewa kwa vyama mbalimbali. Badala yake mrengo huo umependekeza makamishna wateuliwe na kamati huru itakayobuniwa na Tume ya Huduma za Umma, PSC na miungano ya dini.
Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Onyango Oloo amesema  mrengo huo unapendekeza kuwa vipindi vya makamishna visikamilike wakati mmoja. Kamati hiyo awali ilikuwa imeomba muda zaidi wa kujadili mapendekezo yao, jambo lililoifanya kamati hiyo kusitisha shughuli zake kwa zaidi ya saa mbili.