Mbunge wa Kapsaret, Oscur Sudi atalazimika kukaa korokoroni kwa siku nyingine saba ili kuwapa polisi muda wa kufanya uchunguzi kuhusu matamshi ya uchochezi yanayomkabili. Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Nakuru, Joseph Kalu ametoa uamuzi huo akisema Sudi atalazimika kukaa huko hadi atakapotoa uamuzi wa iwapo atamwachilia kwa dhamana ama la.
Tayari mbunge huyo alikuwa amekaa katika seli za Kituo cha Polisi cha Nakuru kwa siku mbili akisubiri uamuzi wa leo wa mahakama wa iwapo ingemwachilia kwa dhamana ama la. Baadhi ya viongozi wa Tangatanga walioandamana na Sudi wakati wa kutolewa kwa uamuzi, wamesema wanaheshimu sheria na kwamba watazingatia maagizo ya mahakama hadi kesi dhidi ya mbunge huyo itakapokamilika. Seneta wa Nakuru, Susan Kihika na Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri ni miongoni mwao.