HUU NDIO MUDA MUAFAKA WA KUUZA MAZAO, GAVANA MRUTTU AAMBIA WAKULIMA

Gavana Mruttu amewashauri wakulima wenye mashamba yanayonyunyiziwa maji kuuza mazoa yao katika msimu huu kufuatia njaa inayolikumba taifa la Kenya. 

Akizungumza na wakulima wa Majengo/Marodo katika wadi ya Mboghoni Taveta, gavana Mruttu alisema kuwa hii ndio nafasi ya kipekee kwa wakulima hawa kufaidika kutokana na bidii yao katika ukulima kufuatia mhemuko wa bei ya vyakula sokoni. 

Vile vile gavana Mruttu amewaomba wafugaji wenye mifugo wengi kuwauza kwani hali ya ukame inakisiwa kuendelea hadi ifikapo mwezi wa kumi na moja.

"Watabiri wa hali ya anga wanasema kuwa ukame huu unaweza kuendelea hadi mwezi wa kumi na moja hivyo basi nawarai muuze mifugo kwani inaweza kufa kwa ukosefu wa maji na lishe," aliongeza gavana.

Shamba za wakulima hawa zimesheheni vitunguu, nyanya, mahindi na ndizi ambazo kwa muda mrefu wakulima wamelalamikia bei duni katika masoko yaliyopo ndani na nje ya Kaunti.