Punguzeni domo domo na vimaneno visivyofaa

Hata kabla ya 2017 kufika, wanasiasa wameanza kujipigia debe na kujitapa hadharani pasi na kutimiza ahadi zao kwa wapiga kura. Joto la kisiasa linalotanda nchini inasambaratisha maendeleo na utendakazi hivyo basi Wakenya watazidi kubakia katika lindi la umaskini. Ubishi kati ya Seneti na Bunge ni dhihirisho tosha kuwa viongozi tuliowachagua wana ubinafsi.

Wabunge wamekuwa joka la mdimu kwa kuzima juhudi za maseneta kujipatia fedha ili kuimarisha jukumu lao la uangalizi wa utendakazi wa serikali za kaunti, Aidha,ukweli wa methali kila mwamba ngozi huvutia kwake umedhihirika kwa sababu wamejitengea bilioni 35 za Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (CDF) hata baada ya marufuku ya hazina hiyo kutangazwa na mahakama.

Baadhi ya viongozi wamegeuka wanafiki, hivi kwamba azimio lao kuu likiwa kujilimbikizia pesa na kujitajirisha huku mkenya wa kawaida akisazwa katika hali ya njaa na pia kuathirika na kipindupindu. Msisimko wa kisiasa unaosheheni nchini ni ushahidi tosha kuwa dhamira ya wanasiasa ni kubaki madarakani zaidi hata kabla ya muhula wao kuisha. Ni vita hivi vya kisiasa na ubabe vinavyotatiza ustawi na utekelezaji wa miradi nchini.

Ni kejeli kwa wananchi kwa kuwa viongozi tulioweka Imani kwao wamegeuka kujitakia makuu, wakidai fedha za maendeleo wanazopata zitatumika katika miradi ya maendeleo huku wakizitumia pesa hizo kujiimarisha kisiasa. Wakenya wamechoshwa na miroromo na mirindimo ya siasa za migawano na kutupia cheche za maneno kwenye mikutano ya hadhara.Yafaa viongozi kuilinda hadhi waliyopewa na wapiga kura na kuasi vimaneno visivyofaa.