Hii hapa ‘checklist’ ya kukagua mpenzi bora

Mapenzi ni kama kikohozi; hayafichiki. Mapenzi haya huwasumbua watu wa rika zote. Kibaya ni kwamba mapenzi hayajui umri, jinsia, tabaka wala kabila. Mapenzi humfanya hata aliyesoma kukaa mbu mbu mbu mzungu wa reli kwa mambo yaliyo bayana na wazi kwamba hayafai wala hayatawahi tokea.

Kwa mfano, harakati za kuwatengesha wapenzi wawili waliojitosa kwenye bahari hii ya mapenzi huwa si kazi kidigo. Utafanya kazi kupita kiasi. Ni kazi ngumu.

Kinachofaa kuangaziwa kwa umakinifu mkubwa zaidi ni kwamba mtu yeyote anapojitosa kwenye mapenzi, hufanya vile ili mahitaji yake yatimizwe.

Mahitaji haya yanaweza kuwa kupendwa, kufurahia maisha, kusafiri, kudekezwa, kutembelea sehemu tofauti tofauti za nchi na mwishowe kufurahia uwepo wa mpenziwe.

Wapo wengi ambao hukosea kwa kuwatafuta wapenzi ambao mahitaji yao hayaambatani na mahitaji yao.
Kwa mfano, mtu anayeandama mpenziwe kwa kuwa ana sura nzuri au ana maumbile ya kuvutia anaweza ishia kujutia matendo yake, kwani mwenziwe anaweza kuwa aliamua kuungana naye ili apate penzi la kweli.

Wawili hawa hata wakiombewa na kumwagiwa anointing oil, hamna linaloweza kuwaleta pamoja ili waishi kwa amani na furaha. Wataishi kuvurugana tu. Wataishi kutatua masaibu yanayowakumba.

Hivyo basi, unapowaona vijana wachanga katika safari ya mapenzi wakiringa na kujishebedua kuhusu jinsi wapenzi wao wanajua kuvalia nguo nadhifu na za kisasa, bila kusahau jinsi wanavyo umbo nzuri, basi tambua kwamba washaanza safari mbaya ya mapenzi. Mwishowe yatawashinda!

Huo ndio ukweli. Mapenzi hayataki papara. Yanataka wawili wanaojua fika kuhusu haja ya kupiga hatua moja baada ya nyingine. Yanataka watu wawili wanaojua kwamba mwenzio akiwa na sura nzuri anaweza kosa umbo nzuri.
Maulana hakumbariki mja awe na vyote. Angelifanya hivi je, umuhimu wa kumchukua mtu mwingine na kumfanya mashuhuri maishani mwako ungetoka wapi?
Babu yangu ameishi kuniambia kwamba, “Mjukuu wangu, hakikisha kwamba hutazami sura wala umbo la mtu. Shughulika na anachokifanya akiwa peke yake wakati hutazami. Skiza mdundo wa mtima wake kwa makini kwani hapo ndipo penye uhondo.”
Maneno haya ya babu yangu kila wakati tukikutana hunikumbusha umuhimu wa kumjua mtu ndani na nje. Nje kunaweza vutia, ila ndani kukawa kumejaa taka. Hamna haja kujizolea taka au kujiletea taka maishani. Kila mja anataka mema, furaha, tabasamu na maelewano na hata wakati haya hayapo, basi utulivu ndio kigezo kikuu cha kuangalia.

Mtu mtulivu ataweza kukuskiza na kabla hajaleta hoja zake atakuwa ametazama. Hii ni mojawapo ya vitu ambavyo vijana wa sasa wanafaa kujifunza. Utulivu husaidia katika mahusiano ya kimapenzi. Endapo hutamwelewa mwenzio kwamba anaweza kuwa na siku mbaya kazini au hata ndugu zake wamempa matatizo, basi ni vyema kuondokea mapenzi.

Vile vile, watu wa kusuasua hawafai kamwe kuwa katika mahusiano. Endapo tabia yako ni ile ya kubabaika kila baada ya sekunde mbili, basi mwachilie mpenzio aende kwa mtu bora. Wewe jikalie hapo ujichongee sanamu uiite mume au mke wako.

Mapenzi bora ni yale ya kumwonyesha laazizi wako kwamba unamwamini, na hata aendapo kazini na kutangamana na watu wengine, unaamini kwamba umpeacho hawezi kukipata kwingine.

Naam! Hayo ndio mapenzi ya kweli, wachana na visanga na vituko uonavyo mitandaoni ambapo watu wanakimbizana kulia na kushoto wakisemezana mabaya kuhusu jinsi wapenzi wao wanachelewa kufika nyumbani. Mwamini mpenzio.

Mwache aranderande, au hata ukitaka - atange tange. Atakaporudi nyumbani utajua kwamba kweli ndege wako unamlisha vinono. Ila chunga usiwe mtu ambaye huwezi kamwe kumlinda ndege wako na anataka kutoka kiotani kila baada ya muda mfupi.

Facebook: Stephen N Mburu
Twitter: MwandishiMburu

Related Topics

Mapenzi