Na Sophia Chinyezi
Takriban nusu ya kesi za ufisadi zinazochunguzwa na Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC zinahusu serikali za kaunti. Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Halakhe Waqo ameieleza Kamati ya Seneti ya Sheria na Haki za Binaadamu kwamba ufisadi umekithiri katika maeneo ya mashinani na kufichua kuwa miongoni mwa kesi mia nne kumi na moja, mia mbili zinazochunguzwa kwa sasa zinahusu kaunti.
Hata hivyo EACC imejivunia kuwa na mwaka wa mafanikio ambapo imewafungulia mashtaka washukiwa kumi na wanane na kushinda rufaa miongoni mwa kesi ishirini na mbili ambazo zimekamilishwa mahakamani.
Wakati uo huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Amos Wako amemwagiza Halakhe kuwasilisha kesi mahakamani kuzishinikiza serikali za kaunti kufuata kanuni za uongozi na maadili kwa maafisa wa serikali kabla ya uchaguzi mkuu Agosti 8 mwaka ujao.