Mgogoro wa mamlaka ikulu

Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Taasisi ya Rais ni afisi inayomilikiwa na maafi sa wawili waliolishwa kiapo cha kuwatumikia Wakenya kwa pamoja pasi na tofauti zozote.

Rais na naibu wake ni marafiki wa tangu jadi kisiasa. Yamkini katiba ya Kenya 2010 haikutabiri uwezekano wa kutokea mzozo kati ya maafi sa hao wawili katika afi si hii.

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto licha ya kuwekwa pamoja na kiapo cha kuhudumu kama Rais na Naibu wake, misimamo yao ya kibinafsi kuhusu maswala tanzu ya kisiasa na ndoto zao za baadaye zimedhihirika wazi katika kipindi cha muhula wao wa pili, ingawaje wote kwa pamoja wakionekana hadharani huvalia nyuso zilizo na maandishi ‘tuko pamoja’ lakini hilo ni kweli?

Baada ya ujio wa Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kwenye serikali kupitia mpango wa “Handisheki” ama kujenga madaraja ya uwiano wa kitaifa na kuzika tofauti za kisiasa baina yao, athari za ushirikiano huo zimejitokeza wazi miongoni mwa vikosi viwili, cha Rais na kile cha Naibu wake.

Sauti ya Rais na Naibu wake kwa wale wanaohudumu katika nyadhifa mbali mbali serikalini inatakiwa iwe moja na yenye mamlaka juu yao.

Nguvu za afi si ya Rais zimekuwa zikikejeliwa mara nyingi kutokana na kukinzana kwa maagizo ya Rais na yale ya makamu wake kwa Waziri Dr. Fred Matiangi na Katibu wa wizara hiyo Karanja Kibicho.

Naibu wa Rais kwa wakati mmoja amekosa kupokea ulinzi wa serikali katika mkutano wake Kaskazini Mashariki mwa nchi, jambo ambalo limevutia kejeli ya hali ya juu dhidi ya afi si ya Naibu wa Rais.

Wengi wanahoji kwamba maana ya serikali ni “Siri Kali” na inakuwa vigumu sana kwa raia ama walio nje ya afi si hizi kuu kuelewa uhalisia wa mambo yalivyo.

Huenda ni kweli kuwa kilichoko moyoni mwa Ruto na Uhuru ni vigumu kubaini kwa sasa, lakini inakuaje wandani wa Ruto na Uhuru wamesalia kwenye mashindano ya kisiasa kila mwisho wa juma huku kila upande ukidai kuhujumiwa na upande wa pili.

Kwa wakati mwingine kiongozi wa waliowengi katika Baraza la Seneti, Kipchumba Murkomen amelalamikia kuhusu kutokuwepo katika katiba majukumu ya wazi ya Naibu wa Rais na hivyo kupelekea kutoheshimiwa kwa afi si hiyo na wanajiona kuwa karibu na Rais.

“Ikiwa hatujafahamu majukumu ya Naibu wa Rais kuna haja gani ya kuongezea nyadhifa zingine kuu?’’, Murkomen ameuliza kwa gadhabu.

Mjadala kuhusu kinyanganyiro cha wadhifa wa Rais na Naibu wake umezagaa katika mabunge yote mawili mitandao ya kijamii ikisheheni uvumi kwamba upande wa Rais unapanga kumbandua kiongozi wa waliowengi katika Baraza la Seneta, Kipchumba Murkomen na kumteua Seneta wa Baringo Gideon Moi ambaye anaonekana kufanya kazi kwa karibu na Rais Kenyatta mbali na kumtikisa Naibu wa Rais kwenye makabiliano ya kumiliki kura za eneo Bonde la Ufa ifikapo mwaka 2022.

Aidha hatua ya Rais kuwaondoa kutoka Baraza la Mawaziri wandani wa Naibu wa Rais wakiwemo aliyekuwa waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri aliyeonekana kuimarisha ushawishi wa Ruto katika eneo la Mlima Kenya na badala yake kumteu Peter Munya kushikilia nafasi hiyo imeonekana kusambaratisha zaidi uhusiano ulio dorora kati ya Rais na Naibu wake.

Mijadala ya BBI mashinani inayoongozwa na waziri mkuu mstaafu Raila Odinga na kuthaminiwa na serikali chini ya wizara ya Mambo ya Ndani na Ushirikishi wa Serikali ya Kitaifa imetajwa kuwa jukwaa teule kwa wapinzani wa Naibu Rais kumkabili ana kwa ana huku wakijifi cha nyuma ya uvuli wa kuhamazisha umma kuuunga mkono ripoti ya BBI.

Ingawaje kwenye mahojiano na hutuba zake za moja kwa moja kwa waandishi wa habari Rais Kenyatta anashikilia kwamba utendakazi wake na Naibu wake bado ni thabiti na unazingatia maswala ya maendeleo, kuna kila sababu ya kuwa na wasi wasi kwani mataifa mengi ya kiafrika yametumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na kutokuwepo maelewano kati ya Rais na naibu wake.

Katika nchi jirani ya Sudan Kusini, Uhasiano mbaya kati ya Rais Salva Kir Mayardid na naibu wake Riak Machar umesababisha nchi hiyo kukosa uthabiti hata baaada ya kujitenga na Taifa la Sudan.

Kule Kusini mwa Afrika, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa mmoja wa naibu wake Jenerali Chiwenga anayehisi kutengwa katika teuzi mbali mbali serikalini.

Huku taifa linapojiandaa kubadilisha katiba kama njia ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa rasilmali, ni bayana kwamba taasisi ya rais bado inamiliki nguvu Zaidi ikilinganishwa na taasisi zinginezo kama vile Idara ya Mahakama na Bunge.

Swali ni: Je, yupo kiongozi atakayekubali kushikilia usukani katika cheo cha rais bila mamlaka makubwa?