×
App Icon
The Standard e-Paper
Smart Minds Choose Us
★★★★ - on Play Store
Download App

Ndindi Nyoro asuta serikali kuhusu elimu ya sekondari ya bila malipo

 

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro akizungumza jijini Mombasa, Januari 22, 2026. [Robert Menza, Standard]

Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, ametoa wito kwa serikali ya Kenya kuharakisha utekelezaji wa elimu ya sekondari ya bure kikamilifu, akisema kuwa haki ya kupata elimu lazima ilindwe na isitawaliwe na masuala ya kisiasa.

Akizungumza jijini Mombasa, Nyoro amesema elimu ni nguzo kuu ya mustakabali wa taifa na lazima iwe ya bure, inayopatikana kwa urahisi na yenye kulindwa dhidi ya ushawishi wa kisiasa.


Mbunge huyo alisisitiza kuwa watoto wote wa Kenya wanapaswa kupata fursa sawa ya kielimu bila kujali eneo au hali ya kiuchumi.

Ili kufanikisha azma hiyo, Nyoro alipendekeza kuanzishwa kwa mfuko wa kitaifa wa elimu ya sekondari ambao utafadhili shule za sekondari za kutwa kote nchini, ikiwemo kugharamia mpango wa chakula shuleni.

Kwa mujibu wa pendekezo lake, shilingi bilioni 10 zinaweza kukusanywa kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Maeneo Bunge (CDF), shilingi bilioni 10 kutoka kwa serikali za kaunti kupitia mgao wa mapato, huku serikali ya kitaifa ikichangia fedha za ziada kupitia Wizara ya Elimu.

Nyoro alieleza kuwa Kenya inahitaji takribani shilingi bilioni 15 kila mwaka ili kufanya elimu ya sekondari kuwa bila malipo kikamilifu, akisema kiwango hicho kinaweza kupatikana kwa kuweka kipaumbele sahihi katika matumizi ya rasilimali za umma zilizopo.

Alisema kuwa uwekezaji katika elimu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi.

Mbunge huyo pia alionya dhidi ya mipango ya elimu inayotekelezwa kwa misingi ya majimbo au maeneo bunge, akisema mbinu hiyo inaweza kusababisha tofauti kubwa kati ya wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali.

Badala yake, alitoa wito wa kuwepo kwa mfumo wa kitaifa unaohakikisha usawa na haki katika upatikanaji wa elimu kwa watoto wote wa Kenya.

Wakati uo huo, Nyoro alielezea wasiwasi wake kuhusu pendekezo la kuuza asilimia 15 ya hisa za Serikali ya Kenya katika kampuni ya Safaricom kwa kutumia bei ya sasa ya soko.

Alionya kuwa Safaricom inauzwa kwa thamani ya chini katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE), jambo ambalo linaweza kusababisha taifa kupata hasara kubwa.

Alitaja mifano ya miamala ya hivi karibuni ya ndani na kimataifa ambapo kampuni ziliuzwa kwa bei ya juu zaidi kuliko thamani yao ya soko, akibainisha kuwa bei ya hisa mara nyingi haioneshi thamani halisi ya mali za kimkakati.

Nyoro alihimiza serikali kuzingatia mchakato wa ushindani wa kimataifa katika uuzaji wa hisa hizo ili kuvutia wawekezaji wengi na kupata thamani halisi ya mali hiyo.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, uuzaji wa hisa za Safaricom kupitia zabuni ya kimataifa unaweza kuingizia nchi mapato makubwa zaidi, fedha ambazo zinaweza kuelekezwa katika sekta muhimu kama elimu, miundombinu na afya.

Alisisitiza kuwa hoja yake si ya kisiasa bali inalenga kulinda mali ya umma na kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kuwekeza katika maendeleo ya sasa na ya baadaye ya Kenya.