×
App Icon
The Standard e-Paper
Fearless, Trusted News
★★★★ - on Play Store
Read on the App

Miaka saba tangu shambulizi la kigaidi la Dusit D2

Recce squard combing the Dusit D2 hotel on 15th January, 2018. [File, Standard]

Jiji la Nairobi limeadhimisha kumbukumbu ya miaka saba tangu shambulizi la kigaidi katika jengo la Dusit D2 lililotokea mwaka Januari 15, 2019, kwa shughuli chache zisizo na makeke, huku vyombo vya usalama vikitoa hakikisho kuwa taifa linaendelea kuwa salama.

Takriban watu 21 walipoteza maisha baada ya magaidi kuvamia jengo la Dusit D2,  baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kufariki dakika chache kabla ya mlipuko huo.

Tukio hilo lilisababisha serikali kuchukua hatua kadhaa za mageuzi ya kiusalama, yakilenga kuimarisha usalama wa taifa na kuboresha uratibu miongoni mwa vyombo vinavyohusika na kukabiliana na ugaidi.

Akizungumza Alhamisi, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alisema kuwa taifa la Kenya inaendelea kuwa salama licha ya vitisho vinavyoendelea kutoka kwa makundi ya kigaidi.


Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kuhakikisha usalama wa umma unaimarishwa zaidi.

“Tunaendelea kuomba ushirikiano kutoka kwa wadau wote ili kuhakikisha usalama wetu,” alisema Kanja, akiongeza kuwa vyombo vya usalama vimefanikiwa mara kadhaa kuvuruga njama za mashambulizi ya kigaidi, hasa kutoka kwa kundi la al Shabaab.

Alisema kuna juhudi nyingi zinazoendelea kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unalindwa ipasavyo.

Hatua chanya pia zimeonekana kupitia mfumo wa haki.

Mwaka uliopita, washukiwa wawili, Mohamed Abdi Ali na Hussein Abdille Mohamed walipatikana na hatia katika mashtaka yanayohusiana na ugaidi, yakiwemo kula njama ya kutekeleza shambulizi la kigaidi na kuwezesha kitendo cha kigaidi, kinyume na Kifungu cha 9A cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi.

Mahakama ilibaini kuwa wawili hao walihusika moja kwa moja na shambulio la Dusit D2, ambalo liliacha makumi ya watu wakiwa wamejeruhiwa na wengi kuathirika kisaikolojia.

Katika ushahidi uliowasilishwa mahakamani, ilibainika kuwa mmoja wa washukiwa aliwezesha shambulizi  hilo kwa kutuma Shilingi 836,900 kupitia huduma ya fedha za simu kwa mshirika wake ambaye pia alikuwa mwanachama wa kundi la al Shabaab.

Jaji Diana Kavedza wa Mahakama za Sheria za Kahawa alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake bila kuacha shaka yoyote, akielezea hukumu hiyo kama hatua muhimu katika kuvunja mitandao ya kigaidi na kuimarisha juhudi za kitaifa za kupambana na ugaidi.