Wetangula akana kuhusika na kampuni inayochapisha karatasi za uchaguzi wa Agosti 9

Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula sasa ametishia kuelekea mahakamani akidai kuchafuliwa jina kwa kuhusishwa na biashara ya uchapishaji karatasi za kupigia kura katika uchaguzi wa Agosti 9.

Kwenye taarifa, Wetangula ameyakana madai hayo akisema kamwe hajawahi kufanya biashara yoyote na Tume ya Uchaguzi IEBC.

Kauli yake inajiri kufuatia taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti moja humu nchini iliyomhusisha na kampuni ya Ugiriki iliyopewa tenda hiyo , taarifa ambayo Wetangula amesema ni ya uongo.

Taarifa hiyo iliibuliwa na viongozi wa Chama cha ODM waliodai kwamba mpango huo ni njama ya Muungano wa Kenya Kwanza kufanikisha wizi wa kura. Hata hivyo Wetangula amwataka viongozi hao kukoma kumhusisha na madai hayo na badala yake kujitatulia masaibu ya uchaguzi yanayowakumba.

Imeripotiwa kwamba Joshua ambaye alikuwa akimwakilisha Wetangula alisafiri kuelekea Jijini Athens nchini Ugiriki kukutana na maafisa wa kampuni iliyopewa tenda ya kuchapisha karatasi hizo.

Kwa mujibu wa Wetangula, madai hayo yameibuliwa ili kubadilisha mjadala unaoendelea nchini kuhusu kukithiri kwa ufisadi serikalini, kupanda kwa gharama ya maisha vilevile ukosefu wa usalama kwenye baadhi ya maeneo nchini.

Related Topics

Wetangula