Malumbano yaendelea kati ya mrengo wa Kenya Kwanza na Azimio

Majibizano makali yameendelea baina ya pande za Naibu wa Rais William Ruto na Raila Odinga kuhusu madai ya Ruto na wandani wake kumkosea heshima Rais Uhuru Kenyatta.

Kauli ya Ruto kwamba atabuni kitengo cha mahakama cha kuchunguza miradi iliyofanywa na Kenyatta na kumwajibisha imeendelea kuibua mjadala mkali kutoka kwa wapinzani wake wanaodai kwamba yeye ni mnafiki. 

Aidha hisia mseto zimeendelea kuchipuka kufuatia suala la hivi punde ambapo Ruto amesikika katika kanda moja iliyorekodiwa, akisema nusura amzabe kofi Kenyatta kutokana na msimamo wake baada ya ushindi wao wa mwaka wa 2017 kubatilishwa na mahakama.

Wandani wa Odinga na Kenyatta wamesema Ruto alijisababishia masaibu yake na kuwaonya Wakenya dhidi ya kumchagua.

Hata hivyo, Ruto amepuuza madai hayo akisema uongozi wake utafanya kipaumbele matakwa ya Kenyatta anapostaafu sawa na kukabili hali ya kuingiliwa kwa taasisi za serikali.

Aidha viongozi wa Kenya Kwanza wameendelea kumtetea Ruto wakimlaumu Kenyatta kwa madai ya kumtenga naibu wake licha ya kumuunga mkono.

Chimbuko la malumbano haya ni kauli ya Kenyatta kumsuta vikali Ruto, na kukashifu ahadi zake alizotoa katika manifesto, akisema alishindwa kufanya yale anayoyasema akiwa naibu wa rais.