NA Mike Nyangwoka
Uteuzi wa Waziri wa Masuala ya Kigeni, Amina Mohammed kutwaa uwenyekiti wa Umoja wa Afrika, AU, unazidi kupata uungwaji mkono huku ikiwa bayana kwamba ana nafasi bora ya kuibuka mshindi. Hatua hii inajiri baada ya mataifa wanachama wa COMESA kutangaza kumuunga mkono. Aidha mataifa haya yamewataka wanachama wake kumuunga mkono Yacin Elmi Bouh wa taifa la Djibouti kuwa Naibu Mwenyekiti wa AU.
Katika barua kutoka mataifa hayo 19, COMESA imesema imechukua hatua hiyo ili kudhihirisha ukomavu wa mataifa ya Afrika, duniani.
Juma lililopita, Rais Uhuru Kenyatta akiwa katika mkutano nchini Togo aliwasihi marais wanane kumuunga mkono Balozi Amina.
Mataifa hayo ni pamoja na Kenya, Burundi, Comoros, DR. Congo, Djibouti, Misri, Eritrea, Ethiopia, Libya, Madagascar, Malawi, Mauritius, Rwanda, Ushelisheli, Sudan, Uswizi, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Kwa mujibu wa Naibu wa Rais William Ruto, uteuzi wa Amina Mohammed umetokana imani aliyonayo Rais kwake.