Maafisa wakuu wa vitengo vyote vya usalama katika Kaunti ya Kilifi wamehamishwa.
Waziri wa Usalama na Masuala ya Ndani ya Nchi, Profesa Kithure Kindiki amesema iwapo ni kweli kwamba wapo maafisa waliopokea taarifa kuhusu mauaji ya Shakahola na kukosa kuchukua hatua basi hawastahili kuwa miongoni mwa wanaoendeleza uchunguzi.
Aidha amesema kuhamishwa kwa wakuu hao kutawapa imani wananchi katika uchunguzi unaoendelea akisisitiza watakaohamishwaha wahusishwi kivyovyote na mauaji hayo ya Shakahola.
Miongoni mwa wale ambao wamehamishwa ni wakuu wa Idara ya Polisi, Polisi wa UtawalaAP, Idara ya Upelelezi DCI na Idara ya Ujasusi NIS.
Kindiki aidha amesema serikali imefanyia mabadiliko uongozi wa vitengo vinavyoongoza uchunguzi akisema Idara ya Polisi itawatuma maafisa wa ngazi za juu zaidi Shakahola kuanzia leo hii ili kuongoza katika shughuli hiyo.
Vile vile Profesa Kindiki amesema uchunguzi huo umeimarishwa hata zaidi baada ya maafisa zaidi kutumwa akisema vile vile umepigwa jeki kwani wamelazimika utafanywa hata kupitia angani ili kuweza kulikagua shamba hilo la ekari mia nane kikamilifu.
Viongozi wa eneo la Kilifi wakiongozwa na Gavana Gedeon Mung'aro na Seneta Steward Madzayo wameipongeza hatua ya kuwahamisha wakuu hao wa usalama, wakiomba maafisa ambao wamehudumu katika kaunti hiyo kwa miaka zaidi ya kumi kuhamishiwa kwingineko pia.
Hayo yanajiri huku shughuli ya kuifukua mili iliyotarajiwa kuendelea leo hii ikikosa kufanyika kutokana na mvua kubwa ambayo imenyesha katika eneo hilo.