Siku moja nilikuwa nikititazama mchezo wa Bao la Kiswahili, katika mtaa mmoja wa kiswani wa Mwembe Tanganyika mjini Mombasa. Ni zamani sana, ni mwishoni mwa miaka ya 1960. Maskani hiyo ilikuwa ikihudhuriwa na watu wa makabila yote pasipo kubaguana. Palikuwa hapazungumzwi lugha nyingine zaidi ya Kiswahili. Kati ya waliokuja kucheza bao maskani hiyo, walikuwa wamepiga vita vikuu vya pili vya Dunia vilivyokuwepo kati ya 1939 hadi 1945. Kwa tajriba hiyo tu utaona kuwa maskani hiyo wengi walikuwa watu wazima. Mimi kwa wakati huo nilikuwa kijana wa miaka 24 hivi, nikimfuata babu yangu Mzee Msabila ambaye alikuwa manju katika ufundi wa kulicheza bao hilo. Wenyewe wasema mcheza bao anayeweza kupiga duru saba na kuendelea, huyo ni fundi. Licha ya kuwa na miaka hiyo niliootaja, katika maskani hiyo nilionekana mtoto.
Nilikuwa nikitumwa tumwa, hata kupeleka mahitaji muhimu ya nyumbani kwenye nyumba za wazee hao. Naweza kutumwa nipeleke pesa , kitoweo au mbogamboga, samaki, ama nikanunua sigara, tumbaku aina ya ogoro au niende Mwembe Tayari soko la papa kununua papa na kadhalika. Tena sio kama utapewa asante au pole la, Wazee hao waliamini kwamba unatekeleza wajibu wako. Maskani ya watu wazima na wazee panakuwa na wanautani wao wa asili kati ya kabila Fulani na kabila Fulani. Mfano nilijulia hapo kwamba Mnyamwezi kutoka Tanzania ni mtani wa Mkamba kutoka Kenya. Mjaluo na Muhaya ni watani wa jadi Mdigo na Mnyamwezi, Wanyasa walitaniana na Wazaramo na kadhalika. Kulikuwa na matusi yazungumzwa lakini huwezi kujua kama wazungumza matusi kama huji kufumbua. Maana wali? cha sana sisi vijana tusigundue. Hata wakiwa wanamsema mwenzao ili waje kumkanya, basi watatumia ku? cha tusijue.