Viongozi wa kaunti zote sita wakiongozwa na magavana wao katika mkutano baina yao na Rais Uhuru Kenyatta. Je, lengo lao ni kuyajali maslahi ya mwananchi ama ni tumbo mbele. [Picha: Pambazuko]
Huku athari za sera tata ya serikali kuu kulazimisha usafirishaji mizigo inayowasili bandari ya Mombasa kupakiwa hadi Nairobi kwa njia ya reli ya SGR ikizidi kubainika, mjadala kuhusu hilo unazidi kupamba moto kila uchao. Pigo la uamuzi huo haswa kwa uchumi wa mji wa Mombasa, pamoja na miji mengine kwa jumla inayotegemea mtiririko wa biashara kutokana na usafirishaji makontena kwa njia ya barabara, umekuwa mfano wa zimwi litakalodhuru sehemu hizo kwa muda mrefu siku za usoni. Huku mjadala huo ukiwavuta wadau wa nyanja mbalimbali husika, baadhi yao sasa wanaonekana kutilia shaka hususan uaminifu wa wajumbe wa kisiasa kuambatana na misimamo yao katika suala hili.