Ijumaa iliyopita, taifa liligubikwa na huzuni baada ya Mbunge wa Kibra Ken Odhiambo Okoth kuaga dunia kutokana na saratani ya utumbo. Mbunge huyo mwenye umri wa 41 alikuwa ameugua ugonjwa huo kwa muda mrefu. Alisa? ri Paris, Ufaransa, kwa matibabu zaidi. Yapata siku tatu baadaye, taifa lilipokea tena habari za tanzia kwamba Gavana wa Kaunti ya Bomet, Joyce Laboso, ameaga dunia kutokana na saratani. Alikuwa na umri wa miaka 58.
Kabla ya kifo chake, mwendazake alikuwa nchini India baada ya kutoka Uiengereza ambako alikuwa akipata matibabu kwa muda kabla ya kurudi hospitali ya Nairobi. Mnamo mwezi Aprili mwaka huu, aliyekuwa mwendeshaji wa magari za mbio za Safari aliyekuwa pia mwanawe Rais Mstaafu Moi, Bwana Jonathan Toroitich, aliaga dunia baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu. Miaka mitano iliyopita, mchezaji mashuhuri wa kriketi nchini Emmy Jepng’etich Ruto maarufu kama Jepkriket bintiye aliyekuwa Gavana wa Bomet Bwana Isaac Ruto aliaga dunia mwaka 2014 kutokana na sarati ya damu. Orodha haikomei hapo. Wiki chache tu zilizopita, Mkurugenzi Mkuu Mtandaji wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom Bob Collymore, aliaga dunia nyumbani kwake akiwa anaendelea kupokea matibabu ya ugonjwa wa saratani.