Wengi wenu mkisikia neno uswahilini unajawa na mawazo kwamba, haya ni maeneo ya watu wa hali duni, sehemu zile zinazoitwa Majengo au mitaa ya mabanda. Ni lazima kutakuwa na maisha ya kihuni huni au ukora tena kuna udaku usabasi na uongo. Baadhi huchukua uswahilini ni kwa watu wavivu wanaopenda starehe, watu wakujipenda wataaradhi na kadhalika. Lakini kwa maana kubwa zaidi ya hiyo, uswahilini ni uafrikani, yaani kule wanakoishi waafrika tena wa hali ya kadiri au kwa lugha nzuri watu wenye kipato cha kati wastaarabu na wenye maadili, na miendo yao ya kimaisha. Licha ya hayo, maeneo mengi ya aina hiyo huwa yana msongamano wa watu.
Kwa sababu maisha katika maeneo hayo huwa nafuu kiasi. Kutokana na hali hiyo, wenye pesa wakakuita uswahilini, maana mchanganyiko huo wa makabila tofauti tofauti, dini na desturi unalazimisha wakazi hao kuzungumza kiswahili ndio lugha kuu ya mawasiliano yao, kikifatiwa kidogo na kingereza, kisha makabila yao pale wanapo kuwa wamekutana watu wa kabila moja na wapo mahala fulani pamoja, wanajikuta wanazungumza lugha yao.