Serikali ya Jubilee imejipa sifa mbovu – kutoshauriana na washikadau; huwakurupukia tu kijeshijeshi raia wake kila inapotekeleza jambo. Raia nao kwa kutishika, hutii amri zenyewe kikondoo licha ya kuwa katika giza totoro. Kutoshauriana huku kumewafikisha katika upeo wa udhia wataalamu wa Kiswahili, mimi nikiwamo.
Ni nani aliyebuni jina Huduma Namba? Je, wavuti wa www.bomayangu.go.ke? Maswali haya yananikereketa maini. Kutokana na kisomo changu kidogo cha Kiswahili hadi kiwango cha uzamili, ninaiambia waziwazi serikali kuwa majina haya yana kasoro! Ninafahamu fika kwamba si lazima lugha za matangazo, vilevile kaulimbiu ziwe sahihi kisarufi– almuradi kuna mvuto ‘unaonasa’ makini ya walengwa, pia uchache wa maneno. Hata kuchanganya maneno ya lugha mfano Kiswahili na Kiingereza kunakubalika. Kila mtaalamu wa lugha anaelewa fika ukiushi huu, sikwambii umuhimu wake.