Walio na matatizo ya moyo waathirika pakubwa na ugonjwa wa covid-19

Chama cha Wataalam wa Matatizo ya Moyo na Muungano wa Magonjwa yasiyoweza kuaambukizwa mfano Kisukari na Saratani wamependekeza wagonjwa wa maradhi hayo kuendelea kushughulikiwa pia wakati huu ambapo bajeti imetengewa  janga la korona.

Katika kikao cha mtandaoni,  mashirika hayo yametoa ripoti  kuwa magonjwa hayo husababisha asilimia 50 ya wagonjwa wanaolazwa na asilimia 40 ya wanaofariki dunia hospitalini. 

Aidha yanahofia kwamba wagonjwa hao wanaweza kufariki dunia kwa urahisi wanapoambukizwa virusi vya korona hasa walio na umri wa miaka zaidi ya 60 . Vilevile wanaofariki kufuatia matatizo ya moyo nchini ni kati ya asilimia 6.1 na 8. 

Mtaalaam wa masuala ya Moyo Daktari Elija Ogola, amesema kuwa ugonjwa wa covid-19 unaleta maradhi ya moyo huku walio na maradhi ya moy wakiwa katika hatari  kubwa ya kuambukizwa.

Ripoti hiyo, aidha ilionyesha kwamba asilimia kubwa ya wagonjwa hawatumi dawa zao kama inavyostahili kwani wanahofia kuambukizwa virusi hivyo wanapokwenda hospitalini.

Kwa mujibu wa Afisa katika Wizara ya Afya Ephantus Maree, mikakati dhabiti imewekwa kuwashughulikia wagonjwa wote, huku kila kituo cha afya katika kila Kaunti kikifunguliwa na sheria za kuzuia maambukizi zikitiliwa mkazo.