SRC imeidhinisha malipo ya marupurupu ya mahitaji ya dharura kwa wahudumu wa afya

Wahudumu wa afya kote nchini sasa watapokea marupurupu ya mahitaji ya dharura baada ya Tume ya Kuratibu mishahara ya Wafanyakazi wa Umma SRC kuidhilisha malipo hayo, wakati waa taifa linakabili maambukizi ya virusi vya korona.

Katika Barua yake, Mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich amesema hatua hiyo imeafikiwa baada ya mkutano uliofanywa Aprili tarehe 28 ambapo jumla ya shilingi bilioni tatu, milioni kumi na tatu na elfu mia tatu tisini zimeidhinishwa kwa malipo hayo.

Barua hiyo ambayo aidha iliandikwa wa Waziri wa Fedha Ukur Yattani  na mwenzake wa Afya Mutahi Kagwe, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliff Oparanya na Katibu wa Wizara ya Fedha Julius Muia,  imetoa mwongozo kuhusu jinsi malipo hayo yatakayofanywa.

Madaktari walio chini ya Muungano wa Chama cha Madkatari KMPDU watalipwa marupurupu ya shilingi elfu ishirini

Wauguzi na wahudumu wengine wanaojihusisha moja kwa moja na waathiriwa wa ugonjwa wa COVID-19, watalipwa  shilingi elfu kumi na tano, elfu kumi kwa maafisa wengine kama wale wa afya ya umma, wahudumu wa mochari, na madereva wao na shilingi elfu tano kwa wanaojihusisha na kudumisha usafi na shughuli nyingine kwenye vituo vya afya.

Sio hayo tu SRC imeagiza madaktari kupewa bima ya afya kwa mujibu wa sheria za tume hiyo na mahitaji mengine kama vile ushauri nasaha.

Wahudumu wa kaunti zote arubaini na saba watanufaika vile vile wale wanaofanya kazi katika Hospitali nyingiene chini ya usimamizi wa Serikali Kuu kama vile ile ya Kitaifa ya Kenyatta, Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret , ya Rufaa ya Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Kenyatta na maafisa wa Afya katika taasisi ya uchunguzi wa Matibabu KEMRI.

Marupurupu hayo ni ya miezi mitatu kuanzia Aprili Mosi.