Jumwa adai polisi wa Malindi wamekuwa kero katika kukabili korona

Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa amewakosoa vikali maafisa wa polisi kwenye Kaunti ya Kilifi kwa madai kuwa wanachangia kusambaa kwa virusi vya korona.

Kulingana na Jumwa, maafisa hao wamekuwa wakiwalazimisha wakazi kujifunga kitambaa cha aina yoyote puani na mdomoni wakitishia kuwakamata na kuwafungulia mashtaka.

Kupitia taarifa yake, Jumwa amesema serikali ilipaswa kuweka mikakati ya jinsi itakavyosabambaza maski kwa Wakenya kabla ya kutoa agizo hilo. Amesema baadhi ya vitambaa vinavyotumiwa na Wakenya wengi haviafikia viwango vya Shirika la Afya Duniani WHO.

Wakati uo huo, Jumwa ameitaka Idara ya Usalama kwenye Kaunti ya Kilifi kuwajibika  wakati wa kutekeleza maagizo ya serikali ya kukabili korona. Amesema licha ya asilimia kubwa ya wakazi wa Eneo Bunge la Malindi hasa wahudumu wa bodaboda kuzingatia maagizo yaliyowekwa na serikali, maafisa wa polisi wamekuwa wakiitisha hongo.

Aidha amewatetea wahudumu wa bodaboda wanaodaiwa kumshambulia Kamanda wa Polisi mjini Malindi George Naibei, akisema walichukua hatua hiyo baada ya kulazimishwa kutoa hongo.