Shughuli zimesitishwa katika Shirika la NYS kufuatia hofu ya Korona

Shughuli za kawaida zimesitishwa katika Shirika la Kutoa Huduma za Vijana, NYS huku wanafunzi wakiagizwa kutoendelea na utaratibu wa kawaida wa masomo katika juhudi za kukabili maambukizi ya Virusi vya Korona.

Taasisi zote za kutoa mafunzo kwa vijana wa NYS zimeagizwa kusitisha shughuli za kawaida huku wakufunzi na wanafunzi wakiagizwa kusalia katika vitengo vyao na kujiepusha kutangamana. Aidha, wameagizwa kuzingatia usafi miongoni mwao vilevile katika kambi wanaozishi.

Hata hivyo, wanafunzi wa NYS wanaohudumu katika taasisi za kutoa mafunzo ya ufundi anuwai za TVET wameagizwa kuelekea nyumbani na kusubiri maelekezo zaidi kuhusu siku watakayorejea.  

 

Ikumbukwe Waziri wa Elimu, George Magoha alizipa taasisi za kutoa mafunzo hadi siku ya Ijumaa kufunga ili kuepusha kuenea kwa Virusi vya Korona.