Mchango wa Mugabe katika Afrika utadumu milele

Aliyekuwa rais wa nchi ya Zimbabwe marehemu Robert Mugabe. [Picha: Standard]

Kifo cha Robert Mugabe baba wa taifa wa Zimbambwe na mdau mkongwe wa kisiasa Afrika kumezusha mjadala mkubwa miongoni mwa wasomi na wanafalsafa wa kimataifa kumuhusu. Je, Mugabe ametowa mchango gani barani Afrika na duniani kwa jumla? Je, alifaulu ama alishindwa katika azma yake ya ufanisi kwa aliowaongoza? Je, tunaweza kumuhukumu vipi bwana huyu tukitilia maanani mapungufu ya mwanadamu katika dunia ilosheheni changamoto sufufu za kisiasa, kiuchumi na kjamii? Mchanganuzi wa kisiasa pwani Abdulkadir Shtua asema Mugabe alianza vyema lakini mwisho akaharibu kutokana na kutakabari na kugeuka dikteta.

‘Mugabe ni kizazi cha wanasiasa wa jadi wa kiafrika wanaoamini kuwa wasemalo ni sawa na hakuna wa kukosoa ama kuwapinga’ asema Shtua akiongeza kuwa alikuwa sambamba na wenzake kama Kenneth Kaunda wa Zambia, Mzee Jomo Kenyatta (Kenya), Hastings Kamuzu Banda (Malawi) na Julius Nyerere (Tanzania). Ingawa maoni ya Shtua yana uzito fulani lakini pia tunaona kuwa utawala wa kiongozi mmoja jasiri ni muhimu kuleta uwiano wa kitaifa.

 Mugabe akiwa na chama chake cha ZANUPF aliweza kutawala siasa za Zimbabwe kwa miaka mingi.Wazimbabwe walimuona kama m’buyu usiotingishika katika maisha yao. Mugabe alikuwa Zimbambwe na Zimbabwe ilikuwa Mugabe.Aliheshimika , akakubalika na wazimbabwe katika tabu na raha. Mataifa ya kimagharibi hususan Uingereza, Ufaransa na Marekani zilifanya kila njia  ikiwemo propaganda kumpiga vita Mugabe lakini wazimbabwe walisimama kidete kuwa nyuma ya kiongozi wao huyu. Jambo moja nyeti ambalo Mugabe alifanya na ambao halitasahulika ni kurudisha ardhi ya wazimbabwe iloporwa na masetla wa kizungu. Hichi ndicho kiini cha mataifa ya kimagharibi kumchukia na kumpiga vita Mugabe aliyeapa kurudisha heshima ya mtu mweusi alodhulumiwa.

Akiwa anatoka katika kabila kubwa la Ndebele bwana huyu alichukuwa hatua hiyo ambayo hata waanzilishaji wengine wa kitaifa Afrika hawakuthubutu kufanya. Historia ya Zimbabwe inatueleza jinsi gani waafrika walivyopokonywa ardhi yao ya rutba na wazungu waliowafurusha hadi katika ardhi kame isozalisha kitu. Mugabe hakujali vikwazo vya nchi za magharibi ziloghadhabishwa na hatua ya kuwapokonya ardhi wazungu wenzao. Kwa wafrika hatua ya Mugabe iliashiria mwanzo mpya kuwa muafrika aweza kujikombowa kutoka kwa minyororo ya wakoloni.

Ni Mugabe aliyeongoza mikakati ya kuleta uhuru wa Zimbabwe kutoka kwa mkoloni muengereza. Akiwa na chama chake cha ZANU-PF bwana huyu alifanikisha uhuru wa nchi yake. Kupatikana uhuru wa Zimbabwe haikuwa rahisi na Mugabe anastahili kongole kwa ufanisi huu. Aliweza kupambana na vibaraka wa wazungu kama Ndambaningi Sithole na Joshua Nkomo na kushinda. Pengine hatuwezi kuwalaumu wazimbabwe kwa kumng’owa madarakani Mugabe kutokana na umri wake mkubwa na kuteleza kwake katika maamuzi kama kumfanya mke wake mchanga Grace kuwa mtawala.

‘Mugabe wa mwanzo hakuwa Mugabe wa sasa kwani Zimbabwe ilitaka mabadiliko’ asema Shomari Bwanamake mdau wa siasa pwani na kuongeza kuwa sana ikizidi sana si vizuri sana. Kivyovyote vile mchango alotowa Mugabe huko Zimbabwe na Afrika hauwezi kufutika katika kumbukumbu zetu.Amekufa akiwa na miaka 95 mashallahu. Alale pema Comrade ‘Bob’ Aluta Continua!