Amehudumia mkoloni, Jomo Moi, Kibaki na Uhuru: Mnyenze

Mzee Abdallah Ali Mnyenze.

Ni Mzee wa Kaya za kimijikenda zaidi ya 30 mkoani pwani na mwanasiasa mkongwe aliyekutana na maraisi na vigogo nchini tangu 1950. Aliwahi kuteuliwa kama diwani maalum Kwale enzi za raisi mstaafu Mwai Kibaki.

Ni mwana wa Mzee Ali Mnyenze aliyekuwa na mabibi wa nne, ambapo mamake Abdallah Mnyenze, Asha Binti Salim Mrandani alikuwa mke wa tatu.

Mzee Abdallah Mnyenze ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa pwani linalotetea umoja na amani mkoani lenye kuwakilisha kabila zote za pwani Waandishi wa Pambazuko walimtembelea gwiji hili nyumbani kwake Kinondo ya Chale kupata undani wa historia yake ambako walimkuta akisimamia ujenzi wa shule mpya ya chekechea iliyoko katika ploti yake.

SWALI: Wakenya hususani wa pwani wamezoea kumuona Mzee Abdallah Ali Mnyenze kwenye runinga, mikutano, sherehe za kitaifa na maonyesho ya kilimo akiwavika maraisi na wanasiasa maarufu nguo za kitamaduni. Wengi pia humuona akifanya maombi kwenye kaya na wenzake lakini je kuna mengine ambayo hawayajui?

JIBU: Mbali na kuwa mwenyekiti wa kaya zote na baraza la wazee pwani, mimi pia ni mtetezi wa haki za ardhi na turathi za wenyeji nikishirikiana na wizara husika pamoja na shirika la makavazi ya kitaifa nchini. Kwa hilo najivunia kuwa kaya zote zilisajiliwa rasmi 1992 enzi za Kibaki nikishirikiana na mzee Mwakio Ndau na mtaalamu wa kizungu bwana Quinton. Mwaka huo huo nikachaguliwa mwenyekiti wa kaya Kinondo, Chale, Muhaka, Gonja, Ribe, Kambe, Chonyi, Dzombo, Ukunda, Shingwaya, Shonda, Similani, Rabai, Fungo na zenginezo. Nashukuru sasa tuna banda la wageni linalotupa kipato, akaunti ya benki na vipeperushi vya maelezo na picha.

SWALI: Yaonesha umekula chumvi nyingi tangu kuzaliwa 1932 enzi za mkoloni mwingereza nchini Kenya hadi wa leo. Je, ni watu gani mashuhuri uliokutana nao kabla na baada ya Gumzo la uhuru jumba la Lancaster uingereza mwanzoni mwa miaka ya ’60?

JIBU: (Akicheka kwa nguvu na kushika tarbushi yake nyekundu) ndani ya miaka yangu 87 kuna maraisi Jomo Kenyatta, Daniel Arap Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta. Nimefanya kazi na Ronald Gideon Ngala, Jaramogi, Shikuku, Masinde Muliro, Wafula Wabuge, Konchellah, Paul Ngei, Oloitiptip, Charity Ngilu, Martha Karua na Raila. Wengine ni Juma Boi, Mwamzandi, Aish Jeneby, Francis Khamis, JD Msechu, Robert Matano, Mwavumo, Shariff Nassir, Babu Mwinyi, Shakombo, Mwakwere, Jahazi, Abdillahi Nassir na mabalozi, na wakuu wa mikoa, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali. Ikizidi, nimeshirikiana na makao wa raisi wote kumi wa jamuhuri na mawaziri wao.

SWALI: Nini siri ya umaarufu wako?

JIBU: Msimamo, heshima, nidhamu, bidii- na kupenda kujifunza mapya mbali na karibu

SWALI: Kabla kuingia KADU ya Ngala, ulikuwa wapi? Na nini hasa kilokushawishi kujitosa upande wa Kenya African Democratic Union dhidi ya KANU enzi hizo ilihali siasa (chembilecho, Charles Njonjo mkuu wa sharia nyakati wa Moi) ni mchezo mchafu?

JIBU: (Akitabasamu) niliwahi kushikwa jijini Nairobi enzi za ukoloni kwenye msako wa Mau Mau wakati natoka kazini General Bus nilikoajiriwa kama mekanika. Nlikuwa nimeacha kazi hiyo kiwanda cha Associated Kenya Sugar Company Ramisi Kwale, nilikohudumu kwa miaka minne (1942-1946). Kumbuka tayari nilikuwa mzazi wa mtoto mmoja wa mke nliyemuoa 1956. Kufika Eastlands mimi na wenzangu wanane tulitiwa mbaroni na askari wakikoloni ingawa tulikuwa na vipande vya kitambulisho cha kodi ambazo waafrika wote walitakiwa wavae shingoni.

SWALI: Ikawaje?

JIBU: Kufika kituoni kwa mchujo, wenzangu sita wakikuyu wakasukumwa kwa Mau Mau wenzao, wagiriama wawili Yahya na Katana wakaachiliwa huru lakini mimi kwa vile nilikuwa na stakabadhi za udereva na mekanika nikawekwa pembeni kungoja wakubwa. Afisa beberu alipokuja na wenzake alinishawishi sana niingie idara ya polisi nikakubali. Miezi minne na siku kumi baadae nikafuzu chuo cha polisi Kiganjo nikawa dereva kamili wa idara ya usalama ya kikoloni- jambo ambalo lilinifanya nikatembea kote nchini ikiwemo vituo vya Diani, Kilifi na Mbaraki mjini Mombasa. Hii ilinipanua kichwa na kuzibua hisia zangu za uzalendo kutokana na ukatili wa wakoloni na ushujaa wa wakenya waafrika. Nilihudumu hadi 1960 nikajiuzulu na kurudi nyumbani na kukuta vuguvugu la KADU chini ya Ngala limetanda kote pwani huku mkoloni akihanyahanya dhidi ya upinzani wa Mau Mau, Jomo Kenyatta na wenzake. Ni wakati huo ndipo nikaanza kuhudhuria mikutano na harakati za KADU nje Mzee Abdallah Ali Mnyenze na ndani ya pwani haukupita muda nikateuliwa katibu wa KADU eneo la Kwale chini ya mwenyekiti Bakari Kitauro na Karama Suleiman ambapo wawakilishi wote wa KADU mkoani pwani tulikutania kwenye bunge letu la kimajimbo (Regional Assembly) ilokuwa kwenye mjengo wa ikulu ya raisi ya sasa mjini Mombasa

SWALI: Pwani na Mombasa ilikuwaje wakati huo?

JIBU: Ngala, Daniel Moi, Masinde Muliro, Martin Shikuku na wengineo walishuka uwanja wa Tononoka kuhutubia halaiki; malori, pikipiki, baiskeli na mabasi zote zilielekea huko… raisi mdogo wa KADU Daniel Moi alisifu alama ya “mkono wazi” ya KADU kama usawa wa makabila yote nchini akidhihaki ishara ya KANU ya kidole kimoja huku vingine vinne vikifumba kama ishara ya haki kwa wachache huku akisema kilichofichwa na vidole vine.

SWALI: Wadhani Ngala alifanya pupa akasahau KANU ina wenyewe?

JIBU: Ngala hakufanya kosa: ukoloni wa kizungu ni mbaya kuliko serikali ya kizalendo. Wana KADU walipata vyeo serikali kuu ya Kenyatta. Shida ni kuwa viongozi wa pwani serikalini hawakuunganisha uwezo wao kutetea wapwani kwa sauti moja. Mbona jamii zengine kama wamasai, waluhya na wakalenjin zilikuwa KADU na zikaweza kufaidisha watu wao kimamlaka na kimaendeleo kutoka kwa Kenyatta, Moi, Kibaki na Uhuru. Wengi tulitumaini “mgogo wehu” (Ngala) atarithi uraisi kutoka kwa Mzee Kenyatta. Bahati mbaya alifariki ghafla tukabaki njia panda. Sidhani kutazuka Ngala Mwengine ingawa Karisa Maitha alijaribu kidogo. Tatizo la Maitha ni kubwabwaja hovyo kuhusu azma yake hadharani kutaka kuwa raisi baada ya Kibaki hasa kwenye mikutano iliyofanywa Kinango. Alipokufa, pwani kazimia mpaka leo. Hawa viongozi wa sasa ni waoga na hawapendani na wanaujasiri wa ulimi lakini siyo wa moyo.

SWALI: Yaonesha huna Imani na viongozi wa pwani?

JIBU: Shida kubwa ya pwani na wa pwani ni kudandia vyama vya wenzao kutoka bara ambao kila mmoja ana chama chake cha akiba kibindoni. Kalonzo, Raila, Mudavadi, Ruto na hata Uhuru waliunda miungano ya vyama hawakuvunja vyama vyao asilia. Sisi wa pwani, tuliuwa shirikisho party of Kenya na sasa tumebaki wakimbizi wa ODM na Jubilee.

SWALI: Baraza la wazee wa pwani unaloliongoza kwa nini limeshindwa kupatanisha Gavana Joho na Aisha Jumwa upande mmoja na vile vile mzozo wa Gavana Salim Mvurya na MCA wake. Mbona Gema, Luo council of elders na Njuri Ncheke ya Meru wanaelekeza na kuchuja wagombea wakuu siku za kura. Kwa nini kusiwe na kilinge kimoja rasmi badala ya baraza la wazee pwani, Jumuiya ya Kaunti ya Pwani na vikaragosi vyengine jikoni? Kama huku sikugawanya na kuwakanganya wapwani kabla ya uchaguzi mkuu 2022 basi tuuiteje?

JIBU: Wazo la kuunda baraza la wazee pwani ni langu. Niliwafuata Gavana Mruttu wa Taita Taveta, Gavana Amason Kingi wa Kilifi na mwanasiasa wa zamani Anania Mwaboza wote wakakubaliana nami isipokuwa Joho ndo alionekana kupingapinga. Sisi kauli-mbiu yetu ni UMOJA PWANI, AMANI PWANI inajieleza yenyewe. Ikizidi tuliwapelekea magavana wote sita wa pwani kumbukumbu za azimio letu na barua ya usajili wa baraza hili. Sasa wataka tufanyeje Zaidi ya hapo?

SWALI: Unamkumbuka vipi raisi mstaafu Moi?

JIBU: Moi alileta elimu ya ngumbaro ya wazee kwa mara ya kwanza 1979 na maziwa ya watoto shuleni na pia mishahara ilipandishwa

SWALI: Je, Kibaki?

JIBU: Alileta elimu ya bure shule za msingi na kujenga mabarabara ya kisasa kote nchini. Nakumbuka Ukunda Showground, Kibaki aliwasuta wadigo kwa kuuza mashamba “sasa hao mabibi wote mnakwenda kuoa mkiuza ardhi zenu, alafu mnalia uskwota, wewe mzee ndiye mchawi unaroga watoto wako kwa umasikini.

SWALI: Raisi Uhuru Kenyatta anafanya kazi nzuri sana wasemaje?

JIBU: Ndio: alileta pesa za wazee kama mimi, alileta Amani kwa handshake yake na Raila na pia amepanua elimu ya sekondari na kuleta Amani nchini Kenya baada ya vurugu mechi 2018. Isitoshe alinizawadi cheti siku ya Mashujaa Day kama shujaa na pia kulinda uhalali wa kaya zote ikiwemo.