Mwanahabari Mkongwe Mohammed Juma Njuguna amefariki dunia

Mwanahabari Mkongwe wa Radio Citizen, Mohammed Juma Njuguna ameaga dunia. Njuguna amefariki mapema leo katika Nairobi Hospital alipokuwa akipokea matibabu baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Inaarifiwa Njuguna amekuwa akiugua maradhi ya kisukari na shinikizo la damu. Sauti ya Njuguna inatambulika sana katika utangazaji wa soka kwa miaka mingi akitumia kauli  “Kadenge na mpira” .

Mohammed amekuwa  Mkuu wa Uzalishaji wa vipindi katika Kampuni ya Royal Media, wadhfa aliyoshikilia tangu mwaka wa 2016.

Njuguna alianza taaluma yake ya uanahabari katika Kampuni ya KBC mwaka wa 1970, akihudumu katika wadhfa wa uzalishaji vipindi vya redio kabla kupandishwa cheo kuwa mhariri mkuu.

Baadaye alijunga na Idhaa ya BBC Swahili ambapo alihudumu kwa miaka mitatu. Kabla ya kifo chake, Njuguna amekuwa akifanya kazi katika Kampuni ya Royal Media tangu kujiunga nayo mwaka wa 1999.

Njuguna atazikwa mwendo wa saa kumi hii leo katika Makaburi ya Kariokor Muslim kulingana na tamaduni za dini ya Kiislamu.