Shirika la Msalaba Mwekundu limewakabidhi makazi mapya waathiriwa wa mkasa wa kuporomoka

Shirika la Msalaba Mwekundu limewakabidhi makazi mapya waathiriwa wa mkasa wa kuporomoka kwa bwawa la Solai kwenye Kaunti ya Nakuru.  Jumla ya nyumba 37 zimekabidhiwa waathirwa hao ambao sasa wanatarajiwa kuendeleza maisha yao upya baada ya kuhangaika kwa muda tangu kutokea kwa kisa hicho mnamo mwezi Mei mwaka uliopita.  Jumla ya shilingi milioni 37  zilitumika katika ujenzi wa nyumba hizo huku kila moja ikigharimu kima cha shilingi elfu 850. 

 Kila nyumba ina vyumba viwili vya kulala, eneo la kuhifadhi vitu na sebule. Aidha jiko na choo vimejengwa katika upande wa nje wa nyumba hizo. Akizungumza wakati wa kuwakabidhi wakazi nyumba hizo, Naibu Gavana wa Shirika la Msalaba Mwekundu, Pascal Mbeche amesema mradi wa ujenzi wa nyumba sawa na hizo vilevile umetekelezwa kwenye kaunti 28 zilizoathiriwa na mafuruko mwaka uliopita.

Amesema kwa ujumla shilingi bilioni moja zilitumika kufanikisha mradi huo. Ikumbukwe watu 48 walifariki dunia baada ya kuta za Bwawa la Patel kwenye eneo la Solai Kaunti ya Nakuru kuporomoka kufuatia mafuriko huku maji ya bwawa hilo yakivisomba vijiji vilivyokuwa karibu na kusababisha hasara kubwa.