Serikali kuzima laini za simu za wale ambao hawatajisajili kwa Huduma Namba

Vitengo viwili vya serikali leo hii vimetoa maelezo ya kukanganya kuhusu usajili wa Huduma Namba. Muda mfupi baada ya Mamlaka ya Mawasiliano, CA kutoa taarifa kwamba laini zote za simu za wale ambao hawatakuwa wamejisajiliwa kupata Huduma Namba zitafungwa kufikia tarehe 15 Mei, kitengo kingine cha serikali kimejitokeza na kauli tofauti. Msimamizi wa Kitengo cha Kufanikisha Miradi ya Serikali ya Jubilee katika ofisi ya Rais, Presidential Delivery Unit, Nzioka Waita amesema kuwa hakuna Mkenya atakayelazimishwa kujisali kwa Huduma Namba. Katika ujumbe wake wa twitter, Nzioka amesema hitaji hili linaendana na agizo la mahakama kwamba yeyote asilazimishwe kusajiliwa kupata Huduma Namba.

Ujumbe wake wa twitter ulijiri baada ya kauli ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini, CA, Francis Wangusi kwamba laini za watakaokosa kujisajili baada ya muda uliowekwa kukamilika zitazimwa, hivyo kutopata huduma kama vile kutuma na kupokea pesa za M-pesa, Airtel Money na hata kutoa pesa katika benki wakitumia kadi za ATM.

Akizungumza mjini Kisumu Wangusi amesema baada ya muda huo kukamilika, watawasiliana na kampuni za mawasiliano kuwasaidia katika kuzifunga laini za wale ambao watakiuka agizo la serikali kuwataka kujisajili.

Amesisitiza kwamba mpango wa Huduma Namba unalenga kurahisisha huduma za serikali katika kuwakabili walaghai.

Mpango wa Huduma Namba ulizinduliwa wiki mbili zilizopita na unaendelea kwenye maeneo yote nchini. Jumla ya watu milioni nane wamesajiliwa kufikia sasa.

Related Topics

Huduma Namba Simu