Msichojua kati ya Joho na Aisha

Gavana Joho na Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa. 

Wengi juzi walishangaa na kupigwa na butwaa kuwaona wanasiasa wawili mashuhuri wa pwani, Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho na mbunge wa Malindi anayeng’ong’ongwa na chama cha ODM Aisha Jumwa wakikumbatiana kama pwagu na pwaguzi mjini Malindi wakiduwaa kama kweli kunao uhasama wa kisiasa baina yao.

Wafuasi wa pande zote mbili, wanaoshinikiza Jumwa kusukumwa pembeni na wale wanamtetea kwamba anaonewa na chama hawafahamu kwamba wanasiasa wote ni sungura wajanja wakitegemea msemo mmoja kwamba katika siasa hamna hadui ama rafiki wa kudumu.

Gavana Joho ambaye ni mfuasi wa mambo ya kileo sawia na gavana mwenza wa Kilifi Amason Kingi, walijumuika pamoja na viongozi wengine wanaohusudu maonyesho ya vichekesho na ngoma za kuruka majoka (densi) kwenye ukumbi mmoja wa Malindi alipopata fursa ya kukutana ana kwa ana na mbunge mwenyeji wa Malindi, Aisha Jumwa. Wote inaaminika walishindwa kujizuia hivyo wakakumbatiana kwa uzito wa kumbukumbu yao ya miaka mingi katika uhusiano wao wa kisiasa.

Mlezi wa kisiasa

Mengi yamezunguzwa baina ya uhusiano aidha wa kisiasa, ule wa makalameni na hata urafiki wa kufa na kuzikana kisiasa kati ya Gavana Joho na Aisha Jumwa lakini hakuna mwangaza uliowamwilika kimasomaso kutoa jawabu kamili. Ukweli unaofahamika ni kuwa ubunge wa Aisha Jumwa kunyakua kiti cha Malindi katika uchaguzi mkuu uliopita wa Agosti 2017, ulichangiwa pakubwa na Joho baada ya usimamizi wa chama cha ODM kuhakikisha kwamba kambi nyingine iliyoongozwa na gavana wa Kilifi Amason Kingi na seneta Stewart Madzayo imesambarika kiubunge huo wa Malindi.

Joho alipeperusha bendera ya Jumwa na mwakilishi wa sasa wa kina mama wa kaunti ya Kilifi, Getrude Mbeyu ambaye ni mkaribu wa Jumwa ilhali Kingi alikuwa na mlolongo wake wa Juliet Riziki Baya kama mtakiwa wa mwakilishi wa kina mama na Willy Mtengo kama mbunge mtarajiwa wakati huo alipokuwa akitetea kiti cha ubunge wa Malindi.

Nipe nikupe

Wale ambao wanawajua wanasiasa hawa wawili kwa muda mrefu tangu 2013 wakati Jumwa akiwa mwakilishi wa kina mama wa kaunti na Joho akiwa kwenye muhula wake wa kwanza kama gavana wa Mombasa, kamwe hawawezi kushangazwa na mkumbatiano huo wa juzi licha ya majibizano yao makali ya kisiasa kuhusiana na kesi inayoendelea sasa dhidi ya kutimuliwa kwake chamani.

Msishangae, Joho na Jumwa ni warabu wa Pemba wanaojuana vyema kwa vilemba vya kisiasa. Duku duku zaidi ni kwamba mbali na Aisha kufadhiliwa kisiasa za 2013 na 2017 na gavana Joho, zaidi ya hapo pia yakadirika kuwa aliongezewa siyo chini ya shilingi milioni moja kwenye mfuko wa ujenzi wa nyumba yake ya kifahari ya Kakuyuni, Malindi.

Wanasiasa hawa wawili walikuwa na uhusiano wa kisiasa mzuri wa kupindukia kati yam waka 2014 na 2016 wakati Gavana Joho alikuwa ngangari kinyama kukabiliana na serikali ya Uhuru Kenyatta na William Ruto huku mheshimiwa Jumwa naye akiwa nguzo ya kumkinga kinara wa chama Raila Odinga. Inakumbukwa aliwekwa korokoroni kwa kumtetea ‘Baba’.

Ni nyakati hizo ambapo alifaidi pia ushirikiano mwema na gavana na kulingana na mndani wa masuala haya, ni siku hizo ambapo alipata siyo tu misaada ya kimawazo bali pia kusombezwa kwa kiwango kidogo cha ujenzi wa nyumba yake.

Kitanzi cha kisiasa

Leo hii hata wawili hawa wakikumbatiana mbele ya umati kama ilivyodhihirika juzi Malindi, ukweli ni kwamba maji yamekwisha kumwagika na kuzoleka, itakuwa ngumu kwa Jumwa. Kisiasa, Joho hakuwa na budi ila kuonyesha jino kwa sababu jino ni mfupa ilhali ufizi ni nyama.

Hapa kazi ipo endapo kutatangazwa uchaguzi mdogo kama katibu wa ODM Edwin Sifuna alivyohakikishia wananchi wa kaunti ya Kilifi alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara kwamba masuala ya iwapo mbunge wa Malindi atasamehewa hakuna kwani chama kimemzika katika kaburi la sahau. Sifuna alionekana kuanza kumpigia debe Willy Mtengo ishara kwamba bao huenda likawa tayari limeshageuzwa kisiasa.

Kisasi njiani

Wadadisi chungu nzima wa siasa na ndimi zake wanasubiri kwa hamu wakati wowote wa kampeini ya Malindi ikianza kwani twajua itakuwa parawanja ya matusi bin matusi. Kulingana na wandani wa chama cha ODM, wanakubali kwamba Jumwa lazima afukuzwe kabisa lakini hali kadhalila wanamtambua kwamba mdomo wake unaweza kutoa nyoka pangoni.

Wasi wasi wake mwingine ni kuwa huenda akamwaga mtama peupe mbele ya umati na wakereketwa wanao mzizimo kwamba anaweza kujilipiza kwa kutaka kuwanyorosha baadhi ya wanasiasa wanaompinga sasa ilhali walicheza rumba naye kati ya 2013 hadi 2018.

“Hapa tunaona mwanasiasa huyu akijitokeza wazi wazi kwa sababu haogopi na wala hana haya ya kutamka lolote mbele ya watu kwamba anaweza kuwaibisha wote ambao labda walimtongoza n ahata kucheza twisti nao mbeleni”, azungumza mfuasi wake mmoja ambaye anasisitiza kwamba lolote linaweza likajitokeza la aina hiyo kama kisasi cha kisiasa.

Kazi ya kiuno

Wakati alipotamka kwamba “kiuno kina kazi” yake alikuwa anajua asemavyo na kwamba licha ya maswaibu yake yanayomkumba sasa, hawezi kukosa kumbukumbu fulani ambaye ameiweka kama silaha yake ya mwisho kuwakomesha wanasiasa wote wa chama cha ODM na Jubilee ambao labda walimvizia na kumnasa ama kumkosa kati ya kipindi chake cha 2013 kama mwakilishi wa kina mama na sasa kama mbunge.

Bahasha ya wote walioghafulika kusakata kiuno naye huenda ikafunguliwa wakati wa kampeini ya uchaguzi mdogo wa Malindi kama silaha yake ya mwisho!