Gavana wa Samburu Moses Kasaine Lenolkulal kwa dhamana ya shilingi milioni 100

 

Mahakama imemwachilia Gavana wa Samburu Moses Kasaine Lenolkulal kwa dhamana ya shilingi milioni 100 pesa taslimu au shilingi milioni 150 na mdhamini wa kiwango sawa na hicho.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Douglas Ogoti amesema Lenolkulal hatatakiwa kuingia katika ofisi za Samburu kwa miezi 24 ili kuruhusu uchunguzi.

Aidha Mkurugenzi wa mfumo wa IPHMIS ameagizwa kutowaruhusu washtakiwa wengine kumi na watatu kutumia fedha za kaunti.

Lenolkulal alikamatwa mapema  na maafisa wa Tume ya Madili na Kukabili Ufisadi, EACC kufuatia agizo la Mkuu wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji ambaye amesema kuna ushahidi wa kutosha wa kumfungulia mashtaka.

Kwa mujibu wa Haji, uchunguzi umebainisha kuwa Lenolkulal amekuwa akifanya biashara na serikali ya Kaunti ya Samburu kwa kuiuzia mafuta ya petroli kupitia kituo cha mafuta cha Oryx Service kuanzia tarehe 27 mwezi Machi mwaka 2013 kufikia sasa.

Katika kipindi hicho, Oryx ilipokea kima cha shilingi milioni 84 kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo na kwamba fedha hizo ziligawanywa kati ya Lenolkulal na mwandani wake kwa jina Hesbon Ndathi.

Michael Mube  Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC. amesema washukiwa wengine kumi na watatu akiwamo Naibu Gavana Julius Leseeto wanatafutwa.