Mfanyabiashara maarufu akamatwa Mombasa

Mfanyabiashara mmoja maarufu jijini Mombasa amefikishwa mahakamani baada ya kunaswa wikendi akiwa na kilo moja ya dawa aina ya heroin zenye thamani ya shilingi milioni 1.5.

Abdul Majid Msallam Timami wa umri wa miaka 47 amefikishwa katika Mahakama ya Mombasa ambapo anasomewa mashtaka dhidi yake.

Kulingana na Idara ya Upelelezi, DCI dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya begi na zilikuwa zikisafirishwa kwa gari aina ya Honda.

Timami anashtumiwa kuwatumia vijana kuziuza dawa hizo, hali ambayo imesababisha wengi wao kukosa kwenda shuleni na badala yake kujiingiza katika biashara haramu ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Aidha ameshtumiwa kumiliki malori makubwa makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki huku akiyatumia katika biashara haramu.

Inaarifiwa amekuwa akiendesha biashara yenyewe kwa kipindi cha mwongo mmoja uliopita katika Eneo la Tudor.

Related Topics